Watakiwa kuchangamkia fursa za utunzaji wa mazingira

WADAU mkoani Katavi wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana katika suala zima la utunzaji wa mazingira ili kujikwamua kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Meneja wa maendeleo ya biashara Herman Bashiri alipomwakilisha Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Private Agricultural Sector Support Trust (PASS Trust) katika mwendelezo wa kampeni ya ‘Kijanisha Maisha’ inayoendelea kufanyika katika mikoa mbalimbali nchini.

Bashiri amesema taasisi ya PASS Trust inajishughulisha na kuwezesha wajasiliamali wote waliopo kwenye mnyororo wa kilimo kama ufugaji, uvuvi pamoja na mazao ya misitu.

Amesema lengo la kufanya kampeni hiyo ni kuunga juhudi za serikali katika suala zima la utunzaji wa mazingira hasa kwenye kilimo ambacho ni sehemu kubwa ya kipato cha nchi na pia upande wa ajira kwa watanzania.

“Tunahitaji wadau wetu wote waweze kupata hii taarifa na kuchukua fursa ya hii Kijani shirikishi kwa kuwa ni package maalum iliyoandaliwa kwa watu wote wanaotumia mazingira” amesema Bashiri

Nae Afisa Kilimo Mkoa wa Katavi Faridu Abdallah, alipomwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Katavi amesema Mkoa huo una fursa pana ambazo bado hazijaweza kutumika katika sekta ya kilimo hivyo ametoa wito kwa wadau kuzichangamkia fursa hizo.

“Tuna eneo ambalo linafaa kwa kilimo zaidi ya hekta 932,136 lakini eneo ambalo linalimwa hadi sasa ni takribani hekta 250,000 kwa hiyo bado unaona kuna eneo kubwa halijalimwa” amesema Faridu

Amesema serikali imewekeza fedha kwa ajili ya sekta ya kilimo ambapo kwa Mkoa wa Katavi umetenga shilingi bilioni 48 kwa ajili ya uboreshaji wa skimu za umwagiliaji.

Amesema kwa upande wa Sekta ya mifugo na uvuvi kuna ziwa Tanganyika ambalo halijaweza kutumika vizuri ili kutoa matokeo.

“Kuna fursa ya ufugaji wa samaki kwenye mabwaya ya asili,tunaweza tukachimba tukafuga kwa sababu kuna potential, tunavyoweza kuchimba tukapata maji tunaweza kufuga samaki”

Hata hivyo amewataka wafugaji kufuga kwa tija na kuachana ufugaji wa kienyeji ili kuboresha ufugaji ikiwemo unenepeshaji huku akisema Mkoa wa Katavi una maeneo mengi ya ufugaji lakini umekuwa ukikabiliwa na changamoto ya ufugaji wa kienyeji.

“Tunafuga labda kwa ajili ya kujiona kwamba tuna ng’ombe nyingi lakini hatujajiweka kibiashara, tunaenda kwenye Kijanisha tuboreshe kwa maana ya kunenepesha ili tuweze kuboresha ufugaji wetu uwe wa tija”

Kwa upande wake mgeni rasmi Katibu Tawala msaidizi sehemu ya Uchumi na Uzalishaji mkoani Katavi, Nehemiah James, alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa huo Mwanamvua Mrindoko amesema uwepo wa PASS Trust mkoani humo utawasaidia wakulima pamoja na wajasiliamali kutumia nafasi ya uwepo wa taassi hiyo kuboresha biashara na kilimo chao kwa kukopa mikopo.

Nao baadhi ya wadau walioshiriki hafla hiyo iliyosheheni mafunzo mbalimbali wamesema mafunzo hayo yatakuwa tija kwao kwa ajili ya kufanya biashara pamoja na kilimo biashara ili kujikomboa kiuchumi kupitia fursa mbalimbali za mikopo walizoambiwa.

PASS Trust inatoa fursa kwa wadau wa kilimo biashara kutoka sekta ya uvuvi, ufugaji, na misitu kupata mikopo kutoka taasisi za fedha kupitia mfumo wa udhamini wa mikopo wa PASS ambapo wajasiliamali hao wana nafasi ya kupata dhamana ya mikopo ya hadi 80%.

 

Habari Zifananazo

Back to top button