Watakiwa kuweka mpango matumizi bora ya ardhi
WATAALAMU wa masuala ya ardhi katika Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi wametakiwa kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yaliyokua ndani ya hifadhi nasasa yamerejeshwa kwa wananchi.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuf wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mtisi Kata ya Sitalike halmashauri hiyo na kusema kuwa lengo ni kuepusha muingiliano wa makazi ya watu na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kilimo katika maeneo hayo.
Amesema vitongoji ambavyo vimetolewa kwenye maeneo ya hifadhi katika kijiji cha mtisi ni Mtisi A, Mtisi B, Mwenge, Mongozo, Msasani, Makutanio, Muungano, Magula na Mjimwema.
Amesema kata ya Sitalike eneo lake kubwa lilikua ndani ya hifadhi ya msitu wa Msaginya na hifadhi ya Taifa Katavi ambapo Rais ameelekeza baadhi ya maeneo ya vitongoji vilivyo ndani ya hifadhi hizo kurudi kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
“Vitongoji vifuatavyo katika kijiji cha Stalike sasa ni rasmi kwa ajili ya shughuli za kibinadamu, Kitongoji cha Igalukilo, Ilangasika, Kabenga, Kiloleni na Stubwike,” amesema Jamila.
Nae Afisa ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Damas Ngasa amesema mpaka sasa tayari wameaanda mpango wa matumizi bora ya ardhi katika eneo la Mtisi na Matandalani kama ilivyoelekezwa.
“Eneo la makazi kwa upande wa barabara kuu ya Mpanda Sumbawanga tumetenga hekali 543, eneo la makazi kwa upande wa hapa makutanio tulipo tumetenga hekali 100, eneo la madani linategemea sehemu ambayo kuna leseni ambazo tayari zimechukuliwa na tumetenga hekali 2028 na eneo la kilimo kwa upande wa Mtisi na Matandalani ni hekali 4661 jumla ni hekali 7233,” amesema Ngasa.
Diwani wa kata ya Stalike Adam Chalamila ameiomba serikali kupeleka huduma za kijami ikiwemo shule, hospitali, maji, barabara na umeme katika maeneo ambayo kwa sasa ni rasmi kwa makazi ya wananchi.
Baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wameishukuru serikali kwa kusikia kilio chao cha kurudisha maeneo hayo kwa wananchi huku wakidai mwanzo iliwaladhimu kutofanya maendeleo kutokana na kuzuiwa kuendeleza shughuli za maendeleo katika maeneo hayo.