Watakiwa kuzingatia weledi, usiri ukusanyaji taarifa
KATIBU Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dk Hashil Abdallah, amewatahadharisha wadadisi na wasimamizi wa utafiti wa shughuli za kiuchumi kuzingatia weledi na usiri mkubwa wakati wa ukusanyaji wa taarifa hizo za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza Dar es Salaam kwenye ufunguzi wa mafunzo ya wadadisi hao zaidi ya 500 kutoka mikoa yote Tanzania Bara yaliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Abdallah alisema kila mmoja anatakiwa ajue amebeba dhima ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan.
“Hatutawavumilia wale watakaotoa taarifa kabla hazijachakatwa na wakibainika tutawachukulia hatua za kisheria kwa hiyo tuna imani mtafanya utafiti kwa usiri na weledi mkubwa,”alisema.
Aliwahimiza wenye viwanda na wafanyakazi watakaofikiwa kuombwa taarifa kutoa ushirikiano kwa ajili ya kupata takwimu sahihi kwa manufaa ya Taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dk Amina Msengwa alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwanoa watafiti hao ili kwenda kufanya utafiti nchi nzima, kujua idadi kamili ya shughuli za kiuchumi kwenye viwanda, shule, maduka na hospitali utakaosaidia katika utekelezaji wa maendeleo ya nchi.
Alisema mara ya mwisho kukusanya tafiti za kiuchumi ni mwaka 2015. Aliongeza baada ya mafunzo hayo, washiriki watafanya kazi hiyo kwa siku 60 katika mikoa yote.
“Taarifa zitasaidia kuthamini na kuchambua mwenendo wa uchumi, tutajua wamiliki na biashara zao, takwimu zitakuja kutumika katika maendeleo ya nchi,”alisema. Mafunzo hayo ya siku tano yalianza Alhamis na yanatarajiwa kuhitimishwa kesho