Wafugaji wametakiwa wasichunge mifugo yao na kuweka maboma ya muda katika eneo la nyayo za Zama Damu wa Kwanza lililopo Kijiji cha Isere Kata ya Laitole ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro
Ombi hilo limetolewa na msimamizi wa eneo hilo la historia ya mambo ya kale, ambaye ni Ofisa Malikale,
Emmanuel Telele wakati akizungumzia umuhimu wa eneo hilo lenye historia kubwa nchini Tanzania hususan katika uhifadhi.
Anasema wenyeji wanachunga mifugo katika eneo hilo kutokana na ukijani wake, lakini wanasahau historia nzuri ya eneo hilo ambalo zipo nyanyo za binadamu wa kale.
“Eneo hilo lina wanyama wengi kama tembo,twiga na wanyama mbalimbali, lakini wafugaji wanafika eneo hilo wakilisha mifugo yao hivyo serikali iendelee kutoa hamasa ya kuwaondoa Ngorongoro kwenda Msomera, ” amesema.
Naye mmoja kati ya wananchi wanaoishi maeneo hayo na kuweka boma la muda, Mopiriki ole Lemomo anakiri uzuri wa eneo hilo katika malisho ndio maana wanapeleka mifugo yao eneo lisiloruhusiwa, hivyo ili kuondoa changamoto kubwa ya mifugo na watu katika eneo hilo wapo tayari kuhamia Msomera ili kupisha uhifadhi uendelee.
“Tuondoke tu maana mifugo yetu inaliwa na wanyama wakali na pia hawa wanyama wakali wakati mwingine wanadhuru binadamu, hivyo hatuoni faida ya kuendelea kukaa ndani ya hifadhi badala yake tupelekwe Msomera wilayani Handeni tuendelee na maisha mapya kule,” amesema.