Watatu wasimamishwa kazi kwa uzembe Mikese

MIKESE: Wizara ya Ujenzi imesimamisha kazi wasimamizi watatu waliofanya uzembe wa kutoshughulikia kuharibika kwa mizani ya kupima magari yakiwa kwenye mwendo (WIM) eneo la Mikese na hivyo kusababisha foleni katika barabara kuu ya Dar es Salaam – Morogoro.
Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega alitoa maelekezo ya kurejeshwa kwa huduma ya mizani hiyo haraka na kusimamishwa kazi kwa watumishi waliohusika na uzembe huo.
“Maelekezo ya Waziri Ulega tayari yamefanyiwa kazi na Wizara, ambapo timu maalumu ya wahandisi na wataalamu wa mizani imeanza kufanya matengenezo ya mifumo yote ikiwemo mfumo wa kupima magari yakiwa kwenye mwendo (Weigh in Motion) kuanzia tarehe 25 Novemba, 2025,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa imetaja wasimamizi hao ni pamoja na Meneja wa mizani kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Makao makuu, Eng. Leonard Mombia, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Eng. John Mkumba na Msamimazi wa mizani Mkoa wa Morogoro, Eng. British Mpeli.



