Watendaji wadaiwa kuisababishia serikali hasara uendeshaji kesi

WATENDAJI wa serikali wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ya kuendesha kesi kwenye vyombo vya ndani na nje kwa uzembe na wengine kuhofia kupoteza nafasi zao.

Wakili Rosan Mbwambo amesema hayo wakati akitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wasuluhishi wanaosikiliza kesi za migogoro ya mikataba ya ujenzi kutoka taasisi za umma na binafsi yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC).

Mafunzo hayo yalishirikisha wanasheria, mawakili wa serikali, wahandisi, wahasibu, wasanifu majengo na wakadiriaji majenzi.

Advertisement

Mbwambo alidai kuwa mikataba mingi ya serikali inayovunjwa au kukiukwa inatokana na kushindwa kusimamia mikataba husika katika hatua za utatuzi.

“Lakini watendaji wa serikali ama kwa uzembe au kuogopa nafasi zao, hawakubali makosa, ili kuangalia jinsi ya kuumaliza mgogoro huo nje, wanaacha serikali inaingia gharama kubwa,” alisema Mbwambo.

Alisema ripoti ya sasa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/2022 imebainishwa wazi kuwa serikali inapoteza fedha kwenye kushughulikia kesi katika vyombo vya uamuzi ambazo zingeweza kumalizwa kwa njia ya usuluhishi.

Wakili wa Serikali Mkuu, Andrew Rugarabamu alisema mafunzo hayo yamemwongezea maarifa kwani migogoro mingi ni vyema ikamalizwa kwa njia ya usuluhishi.

 

/* */