Watoa huduma msaada wa kisheria kupewa mafunzo

DAR ES SALAAM: SERIKALI imezindua mafunzo kwa watoa huduma wa Msaada wa Kisheria ikiwa ni maandalizi ya Kampeni ya Mama Samia inayotarajiwa kuwanufaisha maelfu ya wananchi wa Dar es Salaam.

Mafunzo hayo yanayofanyika kabla ya uzinduzi rasmi wa kampeni hiyo Juni 16, 2025, yamelenga kuwajengea uwezo maofisa na wataalamu wanaotarajiwa kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa jamii, hasa kwa wananchi wa kipato cha chini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo uliofanyika leo Juni 14, 2025, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Miundombinu, Mhandisi Amani Mafuru akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila,amesema kampeni hiyo ni fursa muhimu kwa wananchi kuondokana na kero za kisheria zinazowakwamisha kimaendeleo.

“Kupitia kampeni hii, tunategemea kuona idadi kubwa ya wananchi wakipata msaada wa kisheria bure, jambo litakalowawezesha kutumia muda na rasilimali zao katika shughuli za maendeleo badala ya kushughulika na migogoro isiyokwisha,” amesema Mafuru.

Ameongeza kuwa elimu ya kisheria bado ni changamoto kwa wananchi wengi, hivyo kampeni hiyo inalenga pia kuongeza uelewa na kuwajengea uwezo wananchi kutambua haki zao na namna ya kuzitetea kwa mujibu wa sheria. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Esther Msambazi, amesema kampeni hiyo si tu itahusisha utoaji wa huduma, bali pia itahakikisha takwimu za migogoro na mahitaji ya kisheria zinakusanywa kwa lengo la kuboresha mifumo ya utoaji wa haki nchini.

“Takwimu hizi zitasaidia sana kupanga mikakati ya kitaifa na kimkoa katika kushughulikia migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa, ukatili wa kijinsia na masuala mengine ambayo wananchi wengi wamekuwa wakiyakumbana nayo bila msaada wa kisheria,” amefafanua Msambazi.

Mafunzo hayo yamehusisha kundi mchanganyiko la watoa huduma, wakiwemo mawakili binafsi, mawakili wa serikali, wasaidizi wa kisheria, maafisa ustawi wa jamii, maafisa ardhi, maafisa wa polisi kutoka Dawati la Jinsia, wasajili wasaidizi na maafisa kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi.

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inatarajiwa kuwa ya aina yake, ikilenga kutoa huduma kwa makundi maalum kama wanawake, watoto, wazee, watu wenye ulemavu na wananchi wanaoishi katika mazingira magumu.

Kupitia ushirikiano wa wadau mbalimbali na taasisi za serikali, kampeni hii inaonekana kuwa hatua muhimu katika kuimarisha haki kwa wote na kujenga jamii yenye uelewa wa sheria, usawa na maendeleo endelevu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button