Watoa wito wanaoichafua serikali mitandaoni

TANGA: KIKUNDI cha Amani nchini kimeitaka Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuongeza kasi ya kuwafuatilia na kuwachukulia hatua kali watu wanaojiita wanaharakati wa mitandaoni wanaotumia majukwaa hayo kupotosha ukweli na kuichafua Serikali.
Kauli hiyo imetolewa jijini Tanga na Mwenyekiti wa Kikundi cha Amani nchini, Hassan Hamisi Kubebelwa katika mkutano maalum wa kikundi hicho uliolenga kuhamasisha uzalendo, kuelezea mafanikio ya Serikali na kupongeza utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Rais tangu alipochaguliwa 2025.
Amewaasa wananchi, hususan vijana, kuacha kushawishiwa na watu wanaoshinda kwenye mitandao ya kijamii wakielezea mabaya pekee na kuficha mazuri mengi yanayofanywa na Serikali.
“Lengo la kuja Tanga ni kuwahamasisha wanakikundi wenzetu wasimame kidete kuelezea maendeleo ya miundombinu mkoani hapa na nchi nzima. Tuache kusikiliza upotoshaji wa mitandaoni; Serikali imaleta fedha za mikopo ya asilimia 10 kwenye halmashauri, watu wakope na kujiendeleza badala ya kulalamika,” alisisitiza Kubebelwa.
Akisoma risala ya kikundi hicho, Mjumbe wa Kikundi cha Amani, Rehema Manyama, alisema katika kipindi cha siku 100, Rais ameonyesha dira na uthubutu wa hali ya juu kwa kufanikisha utoaji wa Bima ya Afya kwa wote, kuzalisha ajira kwa vijana 12,000, kutoa mikopo, na kuituliza nchi dhidi ya misukosuko ya kisiasa.
“Rais wetu ameonyesha dira ya kweli. Ndani ya siku 100 ameweza kuimarisha mahusiano ya kimataifa na kutoa fursa za kiuchumi. Tunashauri ngazi za mikoa ziendelee kutoa elimu ya uzalendo na kuimarisha elimu ya amali ili vijana wajiajiri na kuingiza kipato,” amesema Manyama.



