Watoto watatu wa familia moja katika Kitongoji cha Kayenze ‘B’, Kijiji cha Kamilala Kata ya Katuma mkoani Katavi, wamekutwa wamekufa maji katika mto Kamilala walipoenda kuvua samaki.
–
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani amesema tukio hilo lilitokea Julai 17,2023 na kuwataja watoto hao kuwa ni Rusia Lazima (10) mwanafunzi wa darasa la 5, Kabisi Lazima (9) darasa la nne na Makala Lazima (6) darasa la kwanza wote wanafunzi wa shule ya msingi Kamilala.
–
Amesema miili ya watoto hao imefanyiwa uchunguzi na kisha kukabidhiwa kwa familia kwa ajili ya taratibu za mazishi.
–
Katika tukio lingine Bugeni Madirisha (30) mkazi wa Kijiji cha Jilabela, Kata ya Itenka amekutwa akiwa amefariki katika Kijiji cha Tambukareli, Kata ya Majengo Manispaa ya Mpanda huku chanzo kikidaiwa kuwa ni maradhi ya kifua.
–
Kamanda Ngonyani amesema marehemu alikutwa na umauti alipofika mjini Mpanda kwa ajili ya kupata usafiri wa treni, ili kuelekea kwao mkoani Tabora ambapo akiwa Mpanda maradhi ya kifua yalimzidia hadi umauti kumkuta.