Watoto 75 wakutwa na saratani
WATOTO 75 wamegundulika kuugua magonjwa ya saratani za aina mbalimbali katika kituo cha kudhibiti saratani cha Hospitali ya Centre Medico-Chirurgical de Kinindo (CMCK) iliyopo Kinindo tangu Juni 2022.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, watoto waliobainika ni wenye umri kati ya miezi sita na miaka 15 na kuwa, uhaba wa vituo vya taifa vya saratani na madaktari bingwa umekuwa changamoto katika kukabiliana na saratani.
Ilielezwa kuwa watoto 15 wenye saratani wanatibiwa katika kituo hicho na wamekuwa wenye furaha licha ya maumivu ya ndani.
Daktari anayeshughulikia magonjwa ya saratani katika hospitali hiyo, Jean de Dieu Nziyumvira, alisema magonjwa ya saratani kwa watoto bado hayapewi matibabu nchini hapa.
Alitaja aina za saratani zinazosumbua watoto mara kwa mara kuwa ni pamoja na saratani ya figo, saratani ya damu, saratani ya macho na koo na mapafu.
“Kuna idadi kubwa ya vipimo ambavyo hatufanyi hapa nyumbani kwa sababu ya ukosefu wa maabara,” alisema.
Alitoa mwito wa kuwapo kwa uelewa mkubwa kuhusu utambuzi wa mapema, pamoja na ujenzi wa maabara nyingine nchini.
“Wanahitajika madaktari bingwa wengine wa saratani,” alisema na kuongeza kuwa, takwimu za wagonjwa wa saratani bado hazijulikani kutokana na ukosefu wa vituo vya huduma.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), Burundi ina wagonjwa wa saratani zaidi ya 7,900.