Watoto mil 640 duniani wafungishwa ndoa

S HIRIKA la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), limetoa ripoti mpya kuhusu ukatili wa kijinsia inayoonesha bado kuna vitendo vya kikatili vinaendelea kufanywa dhidi ya watoto vikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni.

Aidha, Taasisi hiyo imesema jumla ya watoto milioni 640 wa mataifa mbalimbali chini ya miaka 18 wamebainika kuolewa, Tanzania ikiwepo. Katika ripoti hiyo iliyotolewa Mei 3, mwaka huu imebainisha kuwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini hali ni mbaya zaidi kwani zaidi ya asilimia 32 ya watoto wa kike chini ya miaka 18 wameolewa.

Katika ripoti hiyo, zaidi ya watoto wa kike milioni 50 walioolewa chini ya miaka 18 wanaishi nchini Ethiopia yenye asilimia 17.3, Tanzania inashika nafasi ya pili kwa kuwa na asilimia 5.7, Uganda yenye asilimia 4.7 ya tatu, Msumbiji asilimia 4.4 ya nne na Kenya asilimia 4.2.

Advertisement

Mkurugenzi Mkuu wa Unicef, Catherine Russell katika taarifa yake alisema visababishi vya ndoa za utotoni kwa miaka ya karibuni ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, migogoro, mlipuko wa maradhi ya virusi vya corona (Covid-19).

Ripoti hiyo imebainisha kuwa uchumi umekuwa na mgogoro, hivyo kusababisha sekta nyingine kuathirika ikiwemo za afya, elimu na hiyo imefanya kuwepo na kutoelewana baina ya makundi au nchi na kusababisha vita ya silaha. Alisema changamoto hizo na athari mbaya ya mabadiliko ya tabianchi zimelazimisha familia kutafuta suluhu ya kujifariji ya ndoa za utotoni.

Katika taarifa hiyo imebainisha kuwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 20 hadi 24 ambao waliolewa wakiwa na miaka chini ya 18 wa Ukanda wa Afrika Magharibi na Kati, asilimia 47 ni wale waliotoka familia masikini na asilimia 61 ni wale wasio na elimu na asilimia 41 ni wale wanaoishi maeneo ya vijijini.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa hali ilivyo sasa wasichana zaidi ya milioni 20 katika maeneo hayo wataendelea kuolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18 katika kipindi cha miaka 10 ijayo.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa wasichana wadogo walioolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18 wanapitia mateso katika ndoa na maisha yao na kuwa changamoto za uzazi pingamizi zimeendelea kuwa tishio kwa maisha yao sambamba na ongezeko la vifo vitokanavyo na uzazi.

Wakati taarifa ya Unicef ikibainisha hayo, serikali ya Tanzania imekusudia kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 kuhusu ndoa za utotoni.

Muswada huo umepangwa kuwasilishwa katika Bunge linaloendelea ikiwa ni mapendekezo ya wadau mbalimbali ya muda mrefu wakitaka sheria hiyo ifanyiwe marekebisho ili itambue umri wa mtoto kwa mujibu wa Katiba ya nchi na kuondoa ukinzani uliopo katika sheria hiyo inayotaja umri tofauti.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul hivi karibuni aliliambia Bunge kuwa serikali itapeleka bungeni muswada wa sheria hiyo baada ya kufikishwa kwenye kamati ya Bunge Februari 2021 kufuatia maamuzi ya Mahakama ya Rufani.

2 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *