Watoto wawapeleka polisi wazazi wakipinga kuchapwa

HALI ya usimamizi wa maadili katika kambi za wakimbizi wa Burundi za Nduta wilayani Kibondo na Nyarugusu wilayani Kasulu, ni mbaya kufuatia watoto katika kambi hizo kuwafikisha polisi wazazi wao wakipinga kuchapwa na kukemewa na wazazi wao.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa idara ya wakimbizi Wizara ya Mambo ya  Ndani ya Nchi, Sudi Mwakibasi alipokuwa kwenye ziara ya ujumbe wa viongozi wa serikali ua Burundi waliofanya ziara kutembelea kambi hizo.

Mwakibasi amesema kuwa hali hiyo ya watoto kwenye kambi hizo za wakimbizi imesababisha watoto wengi kuacha shule, ambapo hakuna wazazi wala walimu wanaoweza kuwachukulia hatua kutokana na hilo kuelezwa kuwa haki yao kuamua wanachoona kinawafaa.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani,  Maendeleo ya Jamii na Usalama  wa Burundi, Calinie Mbashurimana (katikati) na ujumbe wake akiwa kwenye kambi ya wakimbizi Nduta Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma alipofanya ziara ya siku mbili mkoani Kigoma . Wa pili Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya wakimbizi Wizara ya Mambo ya Ndani, Sudi Mwakibasi (Picha na Fadhil Abdallah).

Amesema kuwa hayo yametokana na elimu ya kujitambua na kusimamia haki zao inayotolewa na mashirika mbalimbali ya wakimbizi, hali inayoelezwa imevuruga sana taratibu za wazazi kusimamia maadili ya watoto wao kulingana na mila na desturi zao.

Akieleza athari ya jambo hilo, amesema kuwa asilimia kubwa ya watoto hao kwenye kambi  ya wakimbizi ya Nduta yenye watoto 45,000, ambayo ni asilimia 60 ya wakimbizi wote kwenye kambi hiyo hawaendi shule na hawaoni umuhimu wa kwenda na hawataki wazazi wao waingilie uamuzi wao.

Akizungumzia changamoto hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani,  Maendeleo ya Jamii na Usalama  wa Burundi,Calinie Mbashurimana, amesema kuwa suala hilo linavuruga maadili na nidhamu ya watoto ikiwa ni kinyume na mila zao.

Kutokana na hilo amesema kuwa ili watoto hao wasiendelee kuharibika na mafundisho kambini humo, wameitaka UNHCR kuharakisha kuwarudisha nyumbani wakimbizi wa Burundi waliopo mkoani Kigoma.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button