Watoto yatima Busara Orphanage wapewa tabasamu Eid El-Fitr

DAR ES SALAAM: Watoto yatima wapatao 30 kutoka kituo cha Busara Orphanage Center kilichopo Kibada, Kigamboni, wamepata fursa ya kipekee ya kusherehekea Sikukuu ya Eid baada ya kualikwa na uongozi wa Fun City jijini Dar es Salaam.
Mwaliko huo ulikuwa na lengo la kuwapa watoto hao nafasi ya kufurahia sikukuu kama ilivyo kwa watoto wengine katika jamii, huku wakipata uzoefu wa burudani na kujumuika na watu mbalimbali.
Katika tukio hilo, watoto hao walifurahia michezo tofauti za burudani zilizopo Fun City, pamoja na kula na kushiriki shughuli mbalimbali kwa pamoja.
Furaha yao ilionekana wazi kupitia nyuso zao, hali iliyoashiria umuhimu wa kuwajali na kuwapa nafasi sawa watoto wenye mahitaji maalum ili wajisikie sehemu ya jamii.

Akizungumza katika tukio hilo, Meneja Masoko wa Fun City, Khalifa Bakari, alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mchango wa taasisi hiyo kwa jamii, akibainisha kuwa ni muhimu kuwafikia watoto yatima na kuwapa faraja, hasa katika nyakati za sikukuu.
Aliongeza kuwa Fun City itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha makundi yenye uhitaji yanapata msaada na furaha wanayostahili.

Kwa upande wake, mlezi na msimamizi wa watoto hao, Khadija Ally, alitoa wito kwa jamii kuendeleza moyo wa kujitolea kwa kuwasaidia watoto yatima na watu wenye uhitaji bila kusubiri vipindi vya sikukuu pekee.
Alisisitiza kuwa mahitaji yao ni ya kila siku, hivyo ni jukumu la kila mmoja kushiriki katika kuwasaidia na kuwapa matumaini.

Watoto walionufaika na tukio hilo walitoa shukrani zao kwa mwaliko huo, wakieleza kuwa umewaletea furaha kubwa na kuwapa kumbukumbu nzuri ya Sikukuu ya Eid, huku wakihamasisha jamii kuendelea kuwa karibu nao katika maisha yao ya kila siku na kuwapatia mahitaji muhimu ikiwemo na mahitaji ya shule.




