Watu 26 wauawa kwa bomu Nigeria

NIGERIA: TAKRIBAN watu 26 wamefariki dunia baada ya lori walilokuwa wakisafiria kukanyaga bomu la kutegwa ardhini katika barabara ya kijiji cha Furunduma, karibu na mji wa Rann, kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Afisa mmoja wa jeshi la Nigeria amesema kuwa waliouawa ni pamoja na wanaume 16, wanawake wanne na watoto sita. Bomu hilo linadaiwa kuwa miongoni mwa mabaki ya mashambulizi yanayofanywa na makundi ya itikadi kali.
SOMA: Watu 10 wameuawa kimakosa Nigeria
Jimbo la Borno linaendelea kukumbwa na ongezeko la mashambulizi kutoka kwa makundi ya kigaidi, hasa Boko Haram, ambalo limehusika na uasi wa zaidi ya miaka 15, uliosababisha vifo vya watu zaidi ya 40,000 na kuwafanya wengine zaidi ya milioni mbili kuyahama makazi yao.