MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, Profesa Mohamed Janabi amesema hadi sasa watu 60 wamepata huduma ya kuwekewa puto ili kupunguza uzito.
Profesa Janabi alilieleza HabariLEO Dar es Salaam jana kuwa kati ya watu hao, ni mtu mmoja tu lilimshinda, akatolewa na kwamba hilo ni jambo la kawaida.
“Kuwepo kwa huduma ya kupunguza uzito na kupunguza mafuta mwilini ni sehemu ya utalii wa matibabu hivyo tunatarajia kupata watu wengi zaidi,” alisema.
Profesa Janabi anasema utoaji huduma hiyo unahusisha uingizaji wa mrija wa puto kupitia mdomoni, hali itakayopunguza kiwango cha chakula kwa mhusika.
“Tutaweka kwa miezi nane, tutaingiza kupitia mdomoni hadi kwenye tumbo hakuna upasuaji, tutatumia mitambo ifike mahali pake tutajaza dawa linapunguza ukubwa wa tumbo, ukila kidogo utashiba hivyo tunategemea uzito utapungua,” alisema.
Profesa Janabi amesema gharama ya huduma hiyo nje ya nchi inategemea na nchi na kwamba, India ni Sh milioni 15 hadi 20 na Ulaya milioni 30 kwenda juu lakini hapa nchini ni Sh milioni 4 hadi milioni 4.2.
“Ni tiba salama kama tunavyopandikiza figo, uloto na zingine wakitaka kupata huduma hapa ni rahisi,” amesema.
Profesa Janabi alieleza kuwa faida kubwa ni kusaidia kukukinga na magonjwa ya kisukari, kiharusi, moyo, kushindwa kupumua.
Alisema matibabu yatakayotolewa ni siri ya mgonjwa huchukua siku mbili tu.
“Siku ya kwanza unaweza kusikia kama una vidonda vya tumbo lakini baada ya muda utaendelea kawaida, hospitali hatukaribishi watu lakini tunawaomba wale wenye uzito mkubwa wafike kliniki, tuna kliniki ya siku mbili hapa Mloganzila na siku mbili Muhimbili Upanga,” alisema.
Pamoja na hayo alisema pindi mgonjwa anapopatiwa huduma hiyo na kupungua atapata usaidizi wa mtaalamu wa lishe ili asiongeze tena kiwango cha kula na uzito kuongezeka tena.
“Kabla ya kumhudumia tutapima vitu vingine vyote ndio utakuja kupata huduma, faida kubwa ni kitu ambacho baada ya miezi nane tutatoa na hali ya kula kidogo itaendelea na akirudi tabia ya mwanzo anaweza kuwekewa mara nyingine hivyo ni vyema kuweka kiasi,” alisema Profesa Janabi na kuongeza:
“Na matatizo mengine ni ya kurithi, ukiwa na mtoto ana uzito mkubwa mleteni, wakati mwingine unaweza kukuta mtoto amezaliwa na kilo nne watu wakaona ni kitu sahihi kumbe sio kweli.”