Watu 9 mbaroni kwa meno ya tembo

JESHI la Polisi Mkoa wa Katavi, linawashikilia watu tisa  kwa tuhuma mbalimbali,  ikiwemo kukutwa na vipande 16 vya meno ya tembo wakiwa wameviweka kwenye mfuko wa safleti na kuvificha ndani ya nyumba kwa lengo la kuvitafutia wateja.

Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani amesema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Katavi.

Amesema mtuhumiwa Juma Malosa (47)mkazi wa Kotazi, alikamatwa na vipande kumi vya meno hayo na watuhumiwa wengine ambao ni Edes Maridadi (62), Silasi Maiko (19), Julius Msumeno (73) wakazi wa Kabwe walikamatwa na vipande 6 eneo la Kata ya Karema Wilaya ya Tanganyika, mkoani Katavi.

Ngonyani amesema watuhumiwa wengine ni Pius Mbalamwezi (50),  Edward John(49) Godfrey Mwaka (35), Chrispin George (43) na Gerald Mashamba (45) wakazi wa Kijiji cha Muze walikamatwa na silaha mbili aina ya gobori na nyama zidhaniwazo kuwa ni za wanyama pori.

Naye Kaimu Mhifadhi Mkuu Katavi Francis Makaranja amesema nyara hizo zinaonesha ni takriban tembo saba wameuawa katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Katavi.

 

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button