Watumishi mahakama waonywa rushwa, upendeleo

Watumishi mahakama waonywa rushwa, upendeleo

JAJI Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania, Mustepher Siyani amewataka watumishi wa mahakama nchini kutowaangusha Watanzania kwa kuendekeza ubinafsi, rushwa na upendeleo na kuwafanya wananchi kutokua na imani na utendaji wa mahakama.

Siyani ameyasema hayo katika uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Lindi na Songwe, uliofanyika manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.

Amesema kwa uzuri na muonekano wa majengo hayo yawe ni kielelezo cha kutoa huduma bora kwa wananchi, huku akiwakumbusha wanapotumia majengo hayo wakumbuke kuwa yanatokana na kodi za wananchi watakaokuja mbele yao kutafuta haki.

Advertisement

“Kuna kazi ambazo kila mmoja anaweza kuzifanya, lakini uhakimu sio moja ya kazi hizo kwa hiyo ni lazima sana kujipima na kutafakari katika zama hizi tulizonazo mtumishi wa mahakama anapokamatwa au kutuhumiwa kwa rushwa, anachafua na kurudisha nyuma imani ya wananchi wanayopaswa kuwa nayo,” amesema Jaji Siyani.

Amesema hadi kufikia Septemba 2022 mahakama ilikua imefikisha huduma kwa Mahakama za Hakimu Mkazi kwenye mikoa 26 na mahakama katika wilaya 134 kati ya wilaya 139 zilizopo nchini.

Ujenzi wa mahakama za hakimu mkazi katika mikoa mitatu ya Katavi, Lindi na Songwe utasaidia kupunguza umbali wa huduma na zaidi ni kuharakisha kazi ya usikilizaji wa mashauri.

Amesema kabla ya kuanzishwa kwa mahakama ya hakimu mkazi Katavi wananchi zaidi ya 700,000, walilazimika kufuata huduma hiyo katika Mkoa wa Rukwa.

Naye Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda amesema serikali itaendelea kutoa ushirikiano, ili kuhakikisha wanaimarisha miundombinu ya kutolea huduma za haki.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Mpanda, Haidary Sumry, amesema Mkoa wa Katavi bado unakabiliwa na changamoto ya kuhudumiwa na Jaji kutoka Mkoa wa Rukwa, hivyo aliiomba serikali kuona jinsi gani inaweza kutatua changamoto hiyo, ili Mkoa wa Katavi upate jaji atakayeishi katika mkoa huo na kuwahudumia wananchi kwa ukaribu zaidi.