Waua fisi na kuwachoma moto

WAKAZI wa Mtaa wa Mbae Chundi Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani hapa wameua na kuwachoma moto fisi wawili baada ya wanyama hao kuonekana ni tatizo kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo.

Hayo yalielezwa wiki hii na wakazi wa mtaa huo walipozungumza na gazeti hili wakati wa kuwachoma moto fisi hao.

Mkazi wa Mbae Chundi, Masudi Mohamed alisema wamefanya maamuzi hayo kwa mukusudi kwa sababu kila siku fisi hao wanawatia hasara katika mali zao kama vile mifugo na mazao yao yalipo mashambani.

“Wamewachoma moto kutokana na hasira, wamekula sana vitu vyao kama vile mbuzi, ng’ombe, kuku na mahindi mashambani, kwa hiyo wamekuwa waharibifu sana wa mali za watu,” alisema Mohamed.

Mkazi mwingine wa mtaa huo, Salum Issa alisema takribani mwezi sasa, fisi hao wamekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo, kwa hiyo ili waepukane na adha hiyo, waliamua kuwachoma ili kulinda mali zao.

Hata hivyo, aliiomba serikali kuwasaidia kudhibiti changamoto hiyo ya wanyama hao katika maeneo yao kwani inahatarisha usalama wao, mali lakini pia kurudisha nyuma jitihada wanazozifanya kwa ajili ya maendeleo yao.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo, Sada Saidi alikiri kuwepo kwa tatizo hilo mtaani hapo na kusema kuwa tukio la fisi kwa kiasi kikubwa limekuwa likiwaathiri wakazi wa mtaa huo na kuwakosesha amani juu ya mali zao pamoja na usalama wao kwa ujumla.

Hata hivyo, alisema si vema kuua wanyama na kuwachoma moto wanyama hao kinyume cha sheria kwani walitakiwa wasubiri mamlaka husika waje washughulikie tatizo hilo.

Alisema serikali ya mtaa huo tayari imewasilisha taarifa juu ya tatizo hilo la wanyama katika maeneo hayo kwa uongozi wa manispaa, taratibu zinaendelea za kuhakikisha suala hilo linafanyiwa kazi.

Habari Zifananazo

Back to top button