DAR ES SALAAM; MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewapandisha kizimbani washitakiwa wawili wakikabiliwa na mashitaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini kilogramu 62.298.
Washitakiwa hao ni wafanyabiashara; mmoja mkazi wa Kigamboni, Quizbat Shirima(38) na mwingine mkazi wa Kimara Bucha, Linda Massawe (28).
Washitakiwa hao walisomewa mashitaka yao juzi na wakili wa serikali, Cathbert Mbilingi akisaidiana na Alice Nana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu kesi hiyo ilipofikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo.
Mbilingi alidai kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka mawili. Katika mashitaka ya kwanza ni kusafirisha dawa za kulevya.
Ilidaiwa kuwa Juni 9, 2023 maeneo ya Kibada, Wilaya ya Kigamboni, washitakiwa hao walikutwa wakisafirisha dawa aina ya heroini kilo 62.298.
Alidai kuwa katika tarehe na maeneo yaleyale washitakiwa hao walikutwa wakisafirisha dawa aina ya bangi gramu 231.31.
Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Mbilingi alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa hoja za awali. Washitakiwa walirudishwa rumande.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 27, mwaka huu kwa ajili ya kusomwa hoja za awali kwa washitakiwa.