Wazabuni wanolewa matumizi ya moduli mfumo wa NeST

MAMLAKA  ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeendelea na zoezi la kuwajengea uwezo wazabuni kuhusu matumizi ya moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo (NeST).

Akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wazabuni na wadau wa ununuzi wa umma kutoka taasisi za serikali kwa Kanda ya Kaskazini yaliyofanyika Arusha, Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando amewasihi kujifunza matumizi ya moduli hiyo ili  kuitumia kwa ufasaha na kuisaidia serikali kupata thamani halisi ya fedha.

Sando amesema moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki inafaida nyingi kwa wazabuni, taasisi nunuzi na PPAA kwa kuwa inarahisisha zoezi la uwasilishaji na ushughulikiwaji wa malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma.

“Moduli hii ina faida kadhaa zikiwemo kumsaidia mzabuni kutolazimika kufika katika ofisi za taasisi nunuzi au za PPAA ili kuwasilisha lalamiko au rufaa yake na kupunguza gharama na muda kwa wazabuni kwa kuwa hawatatakiwa kusafiri ili kuweza kuwasilisha malalamiko au rufaa zao,”

Amesema katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita , PPAA imeweza kushughulikia mashauri 171 yaliyotokana na michakato mbalimbali ya ununuzi wa umma, ambapo katika mashauri hayo, PPAA ilizuia utoaji tuzo kwa zabuni 36 kwa wazabuni wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika.

Naye Meneja wa Usimamizi wa Rufaa na Huduma za Sheria PPAA, Florida Mapunda amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha wadau wa ununuzi wa umma kuhusu matumizi ya moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo wa NeST katika Kanda ya Kaskazini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button