Wazazi kukamatwa kisa watoto kutembea usiku Mkuranga

MKUU wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasri ametoa onyo kwa kuwakamata wazazi wanaowaruhusu watoto wao kutembea usiku bila ya kuwa na usimamizi wa mtu mzima.

Akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa dua na futari kwa watoto yatima yaliyoandaliwa na kituo cha Firdaus, alisema hali ya usalama kwa watoto sio nzuri kwa wilaya na nchi kwa ujumla.

Alisema mmongonyoko wa maadili na unyanyasaji umekuwa mkubwa hasa wa kingono ikiwemo  kubakwa na kulawitiwa kwa watoto,  hivyo alitaka kila mtoto anayetembea usiku awe na  usimamizi wa mtu mzima na mtoto atakayekutwa akiwa peke yake mzazi au mlezi  atawajibika kwa hilo.

“Hali Kwa sasa sio nzuri hivyo haturuhusu mtoto kutembea usiku bila ya kuwa na usimamizi maalum. Sitaki kila siku kusikia taarifa ya unyanyasaji kwa watoto wa wilaya yangu” alisema.

Alimalizia kwa kusema anatarajia kula sikukuu ya Eid na watoto wote wa kituo hicho cha  Firdaus ili kuonesha upendo wake kwa watoto yatima na waishio mazingira magumu.

Mkurugenzi wa kituo hicho shehe Sharrif Firdaus  kinachohudumia watoto zaidi ya mia moja katika eneo la Kongowe wilaya ya Mkuranga walishukuru kwa mkuu wa wilaya huyo kuweza kuonesha ushirikiano na jamii ya eneo hilo ikiwemo kujitoa katika shughuli zao.

Lakini pia alisema watashirikiana naye dhadi ya mapambano ya unyanyasaji na uvunjifu wa maadili ikiwemo matukio ya ubakaji na ulawiti ambayo yamekuwa yakiendelea hapa nchini na kupigwa vita na viongozi wa taasisi mbalimbali zikiwemo za kidini.

“Kwanza tunashukuru kwakuwa ni jambo ambalo hatukulitegemea kiongozi mkubwa kufika. Na matarajio yetu dua hizi kufanya kila mwaka huvyo tunaomba kuungwa mkono na watu wengine wanaojiweza.

Habari Zifananazo

Back to top button