Wazazi watakiwa kusimamia malezi ya watoto wao

MKUU wa Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, Jamila Yusuph amewasihi wazazi na walezi kuwa, licha ya kubanwa na shughuli za kujiingizia kipato, pia wanao wajibu wa kusimamia malezi ya watoto wao.

Ametoa wito huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika  soko la Kababaye, Kata ya Kazima, wakati akisikiliza kero za wananchi na wafanyabiashara wa soko hilo na wito ameutoa kutokana na vitendo vya ubakaji na ulawiti kushamiri katika jamii.

Amesema matukio ya ulawiti yamezidi kuongezeka katika jamii, huku takwimu zikionesha wanaofanya vitendo hivyo wengi wao ni ndugu wa karibu, hivyo amewahimiza wazazi na walezi kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao, ili kuisaidia jamii kukomesha vitendo hivyo na kuwabaini wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Watoto wetu wa kiume wanafanyiwa ukatili sana, wanalawitiwa na sisi wazazi sio baba sio mama tuko bize, tusipochukua hatua za kulinda watoto wetu wa kiume hali sio nzuri, tutapoteza mwelekeo sisi watu wa Mpanda, niwaombe wakina mama na kina baba muwe mnatenga muda wa kuongea na watoto wenu,” alisema.

Amewatahadharisha wazazi kuwalaza watoto chumba kimoja na watu wazima au kuwalaza watoto peke yao na wageni kwa kuwa hiyo ni hatari na hapo ndipo chimbuko la ulawiti na ubakaji huanzia.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya, ametoa wito kwa wazazi wenye watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kuhakikisha wanawapeleka katika vituo vya afya, ili waweze kupatiwa chanjo za kuwakinga na magonjwa mbalimbali kama surua na polio.

Habari Zifananazo

Back to top button