Wazazi watakiwa kuwapeleka watoto wao shule

MTWARA: RAI imetolewa kwa wazazi na wananchi kwa ujumla mkoani Mtwara kuendelea kutoa ushirikiano katika shughuli zote za maendeleo ya kielimu kwenye maeneo yao ili kuweza kupata maendeleo yanayotarajiwa na kwa wakati.
Hayo yamejiri wakati wa kilele cha Maadhimisho Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2025 yaliyofanyika kimkoa Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya amesema miongoni mwa shughuli hizo za maendeleo ikiwa ni pamoja na wazazi kuwapeleka watoto shule.
Pia katika kuimarisha upatikani wa elimu bora, serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha wanafunzi wa kike na wakiume kushiriki kikamilifu katika kujiendeleza kielimu kupitia mpango wa elimu bila malipo kwa watoto wote wa kike na wa kiume.
Hata hivyo serikali inawatambua na kuwajali wanawake kwa mchango mbalimbali unaofanywa na wanawake wanaoishi mijini na vijijini kwani juhudi mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa katika kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinatatuluwa.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Katibu Tawala Msaidizi mkoani humo Nanjiva Mzunda amesema serikali ya Tanzania inatambua usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake kuwa ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo yenye tija na endelevu kwa jamii.
Mchumi kutoka Kitengo cha Mipango na Uratibu Mkoa wa Mtwara, Lucy Kikweve amezungumzia masuala ya
uwezeshwaji wa Wanawake kiuchumi mkoani humo kwamba wanawake hao wapunguze matumizi yasiyokuwa ya lazima kwani wafanye matumizi kulingana na kiasi ambacho mtu anacho.
“Niwaombe wanawake mjitokeze kukopa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na ile inayotolewa na taasisi mbalimbali na binafsi ili kuendelea kukuza uchumi na familia zetu,”amesisitiza Kikweve
Maadhimisho hayo ya siku ya wanawake mwaka 2025 yanaenda na kauli mbiu inayosema ‘Wanawake na Wasichana 2025 Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji’.



