Shule ya Sekondari Huria ya Ukonga Skillful imehimiza wazazi kutowakatisha tamaa watoto wao kuwa hawawezi pale wanapofanya vibaya katika masomo yao bali kuwatia moyo kwa kuwapa maneno ya faraja ili wajitahidi.
Akizungumza Dar es Salaam katika mahafali ya 18 ya kidato cha nne ya shule hiyo, Muasisi wa Ukonga Skillful Diodorus Tabaro amesema wazazi wengi wana tabia ya kuwavunja moyo watoto matokeo yake na watoto wenyewe hukataa tamaa kwa kuamini kuwa hawawezi, wao ni watu wa kushindwa tu.
Amesema shule hiyo imekuwa ikipokea watoto walioonekana hawawezi darasani na walioshindikana kitabia na kuwatengeneza upya, kwa kuwapa ushauri wa kisaikolojia, kuwa nao karibu kimasomo na kuwahimiza umuhimu wa kumshirikisha Mungu katika masomo yao.
“Tunazo shuhuda za vijana wengi tuliwapokea wakiwa wameshindikana na wengine walikatishwa tamaa hawawezi tulipowatengeza waligeuka kuwa jiwe la msingi kwa kufanya vizuri na kufika vyuo vikuu,”amesema.
Tangu kuanza kwa shule hiyo miaka 18 iliyopita amesema wanajivunia kuwasaidia zaidi ya vijana 700 walioonekana hawawezi kwa kutimiza ndoto zao za kimasomo na kufika elimu ya juu.
Pamoja hayo, amesema shule hiyo imekuwa ikisaidia vijana wengi walioshindwa kulipa ada hasa wale wanaotoka katika mazingira magumu kwa kuhakikisha wanaendelea na masomo na kutimiza ndoto zao kupitia mfuko maalum.
Kwa mujibu wa Tabaro, mwaka huu wameanzisha matawi mengine Mbezi Luis na Tegeta ili kuendelea
kuwanyanyua vijana walioaminishwa hawawezi na kwamba anaiona shule hiyo miaka 10 ijayo ikiendelea kuwa daraja la wanyonge, yenye kubadilisha tabia za vijana kuwa vijana bora kielimu na kitabia.
Jumla wa wahitimu 205 wa Shule hiyo wanatarajia kufanya mitihani ya kidato cha nne mwezi ujao na kuwaasa wanafunzi hao waingie kwenye mitihani wakiwa na mkono wa Mungu.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu kishiriki Cha Dar es Salaam (Duce) Dk Amani Chipalo amesema yeye ni miongoni mwa mashuhuda akishuhudia ndugu zake waliowahi kusoma shuleni hapo wakifanya vizuri.
Amewataka wahitimu hao kuamini kuwa wanaweza na kutumia elimu waliyopewa kufanya vizuri katika mitihani yao.