WAZEE wa Mkoa wa Dar es Salaam wamesema serikali haiwezi kuleta maendeleo kwa wananchi peke yake bila kuwekeza na kushirikiana na sekta binafsi.
Wametaka pia majadiliano yanayoendelea hivi sasa kuhusiana na makubaliano ya awali ya uendelezaji na uendeshaji wa bandari usiwe sababu ya kuwagawa Watanzania.
Mwenyekiti wa Wazee wa Baraza la Ushauri Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Matimbwa ameyasema hayo jana kwa niaba ya wenyeviti wa wazee wa wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam na wazee wengine ambao walishawahi kufanya kazi bandarini, baada ya kufanya ziara kujionea shughuli za bandari na maboresho yanayoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam.
Matimbwa alibainisha kuwa baada ya ziara hiyo bandarini, wameona namna Bandari ya Dar es Salaam ilivyofanya mambo makubwa na itaendelea kufanya mengi mazuri zaidi ya hayo hasa kutokana na uwekezaji mkubwa ambao serikali imefanya kuiboresha.
“Bandari ya Dar es Salaam ni lango la uchumi na kwa taarifa tulizopata asilimia 40 ya mapato ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanatokana na bandarini, lakini mapato hayo hayawezi kuongezeka kama itategemewa serikali tu kuwekeza hivyo lazima sekta binafsi ishirikishwe…mwekezaji ni yupi, ni yule mwenye uwezo,” alisema Matimbwa.
Akitoa mfano, Matimbwa alisema wameshuhudia mitambo miwili imewekwa bandarini hapo ya kushusha na kupandisha makontena kwenye meli na kuwa mashine moja inagharimu Sh bilioni 40 na zinahitajika mashine 10 na ni mabilioni ya fedha serikali peke yake haiwezi.
“Hatuwezi kusema bajeti yote ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ikapelekwa bandarini. Mlisikia bajeti ya Mbarawa, kuna mambo mengi ya uboreshaji miundombinu katika maeneo mbalimbali…kwa mantiki hiyo lazima kushirikisha sekta binafsi… kama kuna wanaotaka kujifunza waje bandarini kujifunza kama sisi tulivyojifunza leo (jana),” aliongeza mwenyekiti huyo.
Kwa mujibu wa Matimbwa, uwekezaji bandarini haujaanza sasa na kutoa mfano enzi hizo bandari hiyo ilikuwa ikijulikana kama Bellbase ambayo ni Kampuni ya Ubelgiji na kisha baadaye TICTS iliyofanya kazi miaka 20 na hadi leo bandari haijauzwa wala maji kukauka.
Kuhusu mjadala unaoendelea sasa juu ya uwezo wa Kampuni ya DP World ya Dubai, alisema hakuna anayepinga ufanisi na utendaji wa kampuni hiyo, na kuongeza kuwa kama wazee wanasikitishwa na mjadala unaoendelea nchini na unaotaka kuwagawa Watanzania.
“Sisi wazee hatupendi na hatutaki suala hili litugawe. Kama tungekubali enzi hizo Waingereza watugawe Tanganyika wala Tanzania isingekuwepo na wala sisi tusingekuwepo hapa leo…umoja wetu Watanzania ndio nguzo yetu, tusikubali kugawanyika,” alieleza Matimbwa.
Aliongeza: “Kama wazee tunasema tumeridhika na hatua mbalimbali za serikali na Rais Samia Suluhu Hassan alizochukua kuhusiana na makubaliano ya awali ya uendelezaji na uendeshaji wa bandari na baadaye kuridhiwa na Bunge.”
Alisema wataalamu, wasomi, wachumi na wananchi wenye mawazo mazuri wawasilishe kwa mamlaka husika ili mwishoni serikali ifanye maamuzi yaliyo sahihi kwa maslahi na maendeleo ya Watanzania.
Wazee hao walitoa wito kwa wananchi kutumia lugha zenye staha wakati wa kuchangia suala hilo na hasa kuepuka kumchafua Rais kwani kufanya hivyo ni Watanzania kujichafua wenyewe na kwamba Watanzania huwa wana staha, wanaelewana na wana umoja.
Kwa upande wa viongozi wa siasa, wazee waliwataka wachangie mjadala huo bila kuchochea wananchi na serikali iwe sikivu kwa kuchukua mawazo ya wasomi, wataalamu na wananchi ili suala hilo likamilike haraka.
“Tunavyozidi kuchelewa washindani wetu watabeba wateja wetu. Kama tulivyoambiwa kuna nchi saba tunazihudumia bandarini kwetu. Lakini kuna bandari ya Mombasa, Kenya na Beira, Msumbiji tukishangaa shangaa kuna nchi zitatukimbia ziende huko… lazima tutambue wakati siye tuko kupingana wenzetu wanatafuta kwenye ufanisi na mwisho wa siku tutatafuta mchawi kumbe wachawi sisi wenyewe,” alisema.
Awali, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho akiwatembeza wazee hao katika gati namba 0 ambalo hutumika kushusha magari na gati namba saba linalotumika kushusha na kupandisha makasha, alimshukuru Rais Samia kwa uwekezaji mkubwa ikiwamo kuweka mitambo miwili ya kisasa ya kushushia makontena hayo na nyingine moja kufungwa Bandari ya Mtwara.
Mrisho alisema katika bandari nyingi kubwa duniani, zinatumia mashine hizo za kisasa zenye uwezo wa kushusha kontena 35 hadi 40 kwa saa, na kwa Tanzania pia mashine hizo zinahitajika nyingi zaidi, lakini serikali haiwezi kuwekeza bajeti yake yote bandarini na ndio maana ushirikiano na sekta binafsi unahitajika.
“Dunia ya sasa teknolojia inakimbiza, ndio maana ni muhimu kushirikiana na sekta binafsi kwa kuingia makubaliano mazuri na ushirikiano wenye afya na manufaa kwa maendeleo ya Watanzania,” alisema Mrisho.