Waziri aagiza mgodi uanze uzalishaji

WAZIRI wa Madini Doto Biteko, ametaka uongozi wa mgodi wa Kampuni ya Williamson Diamond LTD uliopo Mwadui wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, kuanza kazi ya uzalishaji wa madini ya almasi Julai 15, 2023 baada ya kusitisha uzalishaji takribani miezi sita tangu bwawa la maji tope libomoke.
Biteko ameyasema hayo Juni 30, 2023, baada ya kufanya ziara ya kutembelea bwawa la maji tope jipya likiwa na ukubwa wa hekta 57.2 litakalodumu kwa muda wa miaka miwili nusu.
Biteko amesema uzalishaji uanze tarehe hiyo na kibali watapewa Jumanne wiki ijayo kwenye ofisi ya Mhandisi mkuu na kibali cha watu wa bonde la maji kitashughulikiwa.
“Ninawapongeza uongozi wa mgodi huu, serikali ya mkoa na wilaya kwa ushirikiano mzuri mliouonesha, kwani mlisimama hakuna siasa iliyoingizwa na kila mwananchi aliyeathirika kupata haki yake, “alisema Biteko.
Mhandisi Henry Nditi Mkaguzi Mkuu kutoka Tume ya Madini, amemueleza Waziri Biteko kibali kipo muda wowote watakapohitaji, kwani bwawa hilo limeonekana kukamilika kiasi kikubwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Modest Mkude amesema makubaliano yalifanyika siku tatu zilizopita na uongozi wa mgodi wapate kibali na kuanza uzalishaji hakuna mgogoro wowote hali ni shwari na asilimia 96 wameshalipwa fidia kwa walioathirika na tope hapo awali.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniface Butondo, ameishukuru serikali kuchukua hatua na kulisimamia suala hili ambalo limeenda vizuri, kwani mgodi huo umesaidia kunyanyua uchumi wananchi wa wilaya kwa kulipa mapato na kutoa ajira.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Almasi Mwadui, Ayoub Mwenda amesema wao wako tayari kuanza uzalishaji kuanzia wiki ijayo wanachosubiri ni kibali kutoka ofisi za Madini, kwani bwawa hilo limekamilika na mitambo iko vizuri.
Mhandisi Anael Macha kutoka kampuni ya City Engineering amesema bwawa hilo lilianza kutengenezwa mwezi March mwaka huu na Sasa limekamilika litaweza kudumu kwa muda wa miaka miwili na nusu lina ukubwa wa hekta 57.2
Mining Census 2023
Watanzania mnakaribishwa kwenye SENSA ya Madini 2023 yenye lengo la kujua idadi ya migodi Tanzania, Idadi ya wachimbaji au watanzania wanaoshughulika na sekta ya Madini, Hali ya uchimbaji wa madini (zana zitumikazo kwa kila mgodi) na mapendekezo ya mbinu za kuboresha Sekta ya Madini.