Waziri: Ajira serikalini ni vigezo, hakuna upendeleo

Serikali imesisitiza kuwa haitoi ajira kwa kuzingatia maeneo kwani kila mwombaji wa kazi zinazotangazwa Serikalini huchukuliwa kuwa ana haki sawa.

Katika mchakato wa kuwapima waombaji hao, Bunge limeelezwa mapema leo, waombaji wote hupimwa na kuchujwa kwa vigezo vinavyofanana
bila upendeleo wowote.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi Na Utawala Bora), George Simbachawane ametoa maelezo hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kibamba, Issa Mtevu aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali wa kushughulikia malalamiko ya ajira za Kada ya Afya na Elimu kutolewa kwa waombaji wanaotoka maeneo machache ya nchi.

“Mheshimiwa Spika, niwahimize Watanzania wote wenye sifa stahiki kutoka maeneo yote nchini wajitokeze kuomba nafasi za kazi pindi zitakapotangazwa na Mamlaka zinazoshughulikia ajira nchini ili waweze kushindana na waombaji wengine,” Waziri amelieleza Bunge.

Akinukuu kifungu cha 2.1.2 cha Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la 2 la Mwaka 2008 na Kanuni D.

6 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009, ikisomwa kwa pamoja na Kanuni 12 (1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022, Simbachawene amesema ajira kwa nafasi zilizo wazi katika Utumishi wa Umma hujazwa kwa ushindani wa wazi kwa kufanya usaili na kupata washindi katika nafasi husika.

Habari Zifananazo

Back to top button