Waziri asema madalali ni chanzo migogoro ya ardhi

WAZIRI wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Zanzibar, Rahma Kassim Ali amesema asilimia 80 ya migogoro ya ardhi nchini inasababishwa na madalali.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha mawasiliano katika wizara hiyo ilisema madalali wamekuwa wakichangia kutokea kwa migogoro ya ardhi nchini kutokana na uuzaji wa viwanja usiofuata sheria na taratibu zilizowekwa na serikali.

Alisema kwa kuliona hilo, wizara hiyo inaandaa utaratibu maalumu wa kuweza kudhibiti tatizo hilo ambapo limekuwa likirudisha nyuma jitihada za kuleta maendeleo nchini.

Pia aliwataka wananchi na wawekezaji wanapohitaji kununua maeneo wafike katika taasisi husika na kuacha kuwatumia madalali hao.

“Ningependa kuwataka wananchi wanapotaka kununua maeneo kufika taasisi husika iliyowekwa kisheri ili kuepusha kuongezeka kwa migogoro ya ardhi,” alisema.

Katika hatua nyingine, aliwahimiza wananchi waliopewa viwanja na serikali kuviendeleza na kuvidhibiti kwa lengo la kuepusha uvamizi.

Alisema serikali imetoa miezi sita kwa mwananchi kuendeleza eneo lake mara anapopata umiliki rasmi na raia wa kigeni mwaka mmoja, ukishindwa kuliendeleza eneo hilo hurudi serikalini.

“Niwatake wananchi pamoja na raia wa kigeni kuhakikisha wanayaendeleza maeneo kwa mujibu wa sheria iliyowekwa na wasipoyaendeleza kwa muda uliowekwa, maeneo hayo yatarudi serikalini,” alisema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button