Waziri Aweso atoa maagizo changamoto ya maji Kibakwe

SERIKALI imewataka wahandisi wa maji kutekeleza majukumu yao ipasavyo, ili kuondoa tatizo la upatikanaji maji nchini na kuleta hali ya sintofahamu kwa wananchi.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso wakati alipotembelea miradi ya maji iliyopo Jimbo la Kibakwe, Wilaya ya Mpwapwa.

“Niwaombe radhi wananchi, niwaombe sana tusitafute mchawi, hawa wataalamu wetu ndio wanatakiwa kutumia maarifa yao kutekeleza mradi huu kwa kuzingatia hali ya udongo wa eneo hili.

“Nawaagiza mbele yenu, ndani ya mwezi mmoja changamoto zote za eneo hili zipatiwe ufumbuzi, maji yaanze kutoka,” amesema Waziri Aweso.

Pia amemuagiza Mhandisi wa Maji Wilaya ya Mpwapwa, ndani ya mwezi mmoja kusimamia ujenzi, ukarabati na kusambaza sehemu za kuchotea maji, ili kuondoa tatizo la upatikanaji wa maji jimbo la kibakwe.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, ambaye pia ni Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene, aliwasihi wananchi  kutokuwa na imani za kishirikina, kwani itawagawa kuwachelewesha na kusababisha migogoro.

Waziri Aweso amewaahidi wananchi hao kuwa serikali itatimiza wajibu wake na hakuna changamoto yoyote, zaidi ya wataalamu kutimiza wajibu wao kuwawezesha kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza.

 

Habari Zifananazo

Back to top button