Waziri Mabula asherehekea Krismasi na wagonjwa

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula amesherekea sikukuu ya Krismasi na wagonjwa kwa kula nao chakula pamoja na kukabidhi zawadi za Krismasi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Waziri Mabula amekabidhi zawadi hizo leo kwa wagonjwa katika wodi ya watoto walio na changamoto ya lishe na watoto walio na changamoto mbalimbali za kiafya, ikiwemo watoto waliopata ajali za moto na majanga mbalimbali.

“Nimeamua kuja kusherehekea sikukuu na wagonjwa kwa kuleta chakula nilichopika nyumbani kwangu, vinywaji na matunda, kwa sababu najua leo ni sikukuu ya Krisimasi na ushiriki watoto ni muhimu, lakini kuna ambao wameshindwa kusherehekea wakiwa nyumbani kutokana na changamoto mbalimbali za kiafya,” amesema Dk Mabula.

Waziri Mabula ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, ameonesha njia kwa viongozi kusherehekea sikukuu pamoja na wananchi wenye uhitaji, ambapo ametoa huduma ya vyakula kwa mikoa yote nchini kwa ajili ya Krismasi na Mwaka Mpya, ili watu wote waweze kupika na kusherehekea hata kama hawana uwezo kiuchumi.

 

“Na mimi namshukuru sana Mhe. Rais kwa sababu ameonesha njia toka jana mikoa yote amegawa vyakula kwenye vituo vya kulelea watoto kwa ajili ya sikukuu hizi za Krismasi na Mwaka Mpya, na sisi kama wawakilishi wake ni wajibu wetu kuwatembelea wahitaji hasa watoto, ndio maana nimeamua kuja hapa hospitali kula nao sikukuu,” aliongeza Dk Mabula.

Katika ziara hiyo Waziri Mabula aliongozana na Dk Ibenzi Ernest Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma, ambaye amemshukuru Waziri Mabula kwa sadaka yake hiyo, ambayo amesema ni moja katika mchango mkubwa wa mgonjwa kufarijika pale ambapo anaona watu wanamjali.

Dkt. Ibenzi alitumia fursa hiyo kumuomba Waziri Mabula kufikisha shukrani zake kwa Rais Samia kwa mafanikio makubwa ya kuboresha huduma za afya hasa katika upatikanaji wa vifaa tiba na maboresho ya majengo ya utoaji huduma za afya, katika maeneo mbalimbali nchini.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button