Waziri Mkuu aongoza waombolezaji mwili wa mbunge Mbarali

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewaongoza waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Mbarali, Francis Mtega katika uwanja wa mpira wa Chimala, Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya.

Marehemu Mtega alifariki Julai mosi, 2023 kwa ajali ya kugongwa na trekta shambani kwake Mbarali, mkoani Mbeya.

Akizungumza wakati wa mazishi hayo siku ya leo, Julai 4, 2023 Waziri Mkuu Majaliwa aliwaasa wananchi kuenzi mazuri yote aliyofanya marehemu ili iwe alama ya kumuenzi na kumuombea wakati wote.

Advertisement

Aidha, alisema mchango mkubwa alioufanya mbunge huyo katika kusimamia ajenda muhimu za wana-Mbarali na za kitaifa kwa ujumla kipindi cha uhai wake unatambulika na Rais Samia Suluhu Hassan.

Naye, Spika wa bunge Tulia Ackson amesema kuwa bunge limeumizwa na kifo cha Mtega kutokana na mchango wake mkubwa kwa Wana-Mbarali.

“Mheshimiwa Mtega alikuwa mtu mpole, mstaarabu na mfuatiliaji wa ajenda zote za Wana-Mbarali, alikuwa ni mtu mwema.” Alisema Dk Tulia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda amesema kuwa alimfahamu Mtega kutokana na ushujaa na uhodari wake wa namna alivyokuwa akiwatetea wana-Mbarali likiwemo suala la GN.

“Kutokana na juhudi zake, nilikiri kwamba huyu ndiye mwakilishi wa wananchi. Alikuwa ni shujaa, jambo hilo ni zito, halihimiliki lakini tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atutie nguvu.”

Marehemu Mtega alifariki Julai mosi, 2023 kwa ajali ya kugongwa na trekta shambani kwake Mbarali, mkoani Mbeya.

 

2 comments

Comments are closed.