Waziri MKuu amesema kuwa zoezi la kuzima moto uliozuka katika hifadhi ya Mlima Kilimajaro limefanikiwa kwa kiasi kikubwa huku akishukuru wadau mbalimbali walioshiriki katika janga hilo.
Akitoa ripoti maalum Bungeni Dodoma leo asubuhi, Waziri Mkuu amesema jumla ya hekari 33 zimeteketezwa lakini serikali kwa kutumia vyombo vya uhifadhi kama TANAPA, KINAPA na wadau wengine likiwemo Jeshi la Wananchi (JWTZ), Polisi, Skauti na wananchi imefanikiwa kulinda njia ya kupanda mlima huo.
JWTZ ilitoa helkopta mbili pamoja na wanajeshi 878 ambao wamesaidia kuzima moto huo hasa katika maeneo korofi licha ya changamoto mbalimbali kama upepo mkali na mabonde.
Kuhusu mkakati wa kudumu wa kukabiliana na majanga katika eneo hilo na mengine nchini, serikali imejipanga kuimarisha kitengo cha maafa lakini tathmini ya kina itafanyika baada ya zoezi la kuzima moto katika Mlima wa Kilimanjaro.
Baadhi ya wabunge wameishauri Serikali kuweka kambi za kijeshi jirani na hifadhi ili kukabiliana na dharura kama iliyotokea katika Mlima huo.
“Tumepokea ushauri huo, tutaufanyia kazi,” amesema Waziri Mkuu.