MALI: MKUU wa Jeshi wa Mali Kanali Assimi Goita amemfuta kazi Waziri Mkuu wa kiraia Choguel Kokalla Maiga na serikali yake baada ya Maige kufanya ukosoaji wa watawala wa kijeshi.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari nchini humo, Kanali Goita amesema kwa mamlaka aliyopewa ameamua kusitisha majukumu ya waziri mkuu na maafisa wa serikali.
Maiga, ambaye aliteuliwa na jeshi mwaka wa 2021, Jumamosi iliyopita alilaani hadharani ukosefu wa uwazi kuhusiana na kukamilika kwa kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia.
Amesema mkanganyiko huo wa madaraka unaweza kusababisha matatizo makubwa na kuhatarisha nchi kurudi nyuma kimaendeleo.
Tangu nchi hiyo kufanya mapinduzi 2020 na 2021, utawala huo wa kijeshi uliahidi Juni 2022 utaandaa uchaguzi na kukabidhi madaraka kwa raia ifikapo Machi 2024, lakini baadae uliahirisha uchaguzi hadi wakati usiojulikana.