Waziri Ulega aipongeza Tulia Trust
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amepongeza juhudi zinazofanywa na Taasisi ya Tulia Trust kwa kuwezesha vijana kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Waziri Ulega amebainisha hayo leo jijini Mbeya alipofanya ziara katika banda la taasisi hiyo kwenye maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale.
Amesema Spika wa Bunge la Tanzania Dk Tulia Ackson, ambaye ni muasisi wa Tulia Trust amekuwa akifanya jambo jema kwa kushirikiana na serikali kutambua changamoto za wananchi wa Mkoa wa Mbeya kupitia taasisi hiyo na kuwasaidia kuzitatua kwa njia moja au nyingine.
“Tulia Trust ni mfano mzuri wa kuigwa na viongozi na jamii kwa ujumla, imewabadilisha kifikra vijana kupitia maono mbalimbali na kuwainua kiuchumi.
” Kuwaondoa kwenye makundi ambayo hayana tija kwao na kujiepusha na vitendo hatarishi kwenye maisha yao, kumewawezesha vijana kushiriki kazi za ujenzi wa Taifa kwa weledi mkubwa,” amesema
Ameiomba taasisi hiyo kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha inaendelea kuisadia jamii kukabiliana na changamoto mbalimbali hususan zinazowakabili vijana.