WB kujenga njia ya umeme Tanzania, Uganda

BENKI ya Dunia (WB) imetatoa fedha za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo mkubwa wa kilovolti 400 kutoka Uganda hadi Tanzania.
Mtaalam wa Nishati kutoka Ofisi ya Benki ya Dunia nchini Tanzania, Dk Rhonda Jordan ameeeleza hayo wakati alipofanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dodoma.

Dk Rhonda amesema kuwa kwa sasa benki hiyo imeridhia kutekeleza mradi huo baada ya kujiridhisha kuwa hauna athari za kimazingira kama ilivyokuwa ikielezwa hapo awali.
“Bodi ya Wakurugenzi sasa itapitisha fedha kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huu, ambao ulikuwa ukisuasua kutekelezwa kwa madai ya kuathiri mazingira, lakini sasa bodi imeridhika na itatoa fedha za kuanza kuutekeleza,” amesema Dk Rhonda.

Katika hatua nyingine, Dk Rhonda ameialika Wizara ya Nishati kushiriki katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika Jijini New York, Marekani, Septemba 2025.
Katibu Mkuu Mramba amemueleza Dk Rhonda kuwa wataendelea kushirikiana na Benki ya Dunia katika miradi mbalimbali ya Nishati ukiwemo wa usafirishaji umeme wa Tanzania-Zambia (TAZA) na mingine kama hiyo.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Innocent Luoga na Mhandisi Nishati Mkuu, John Mageni.



