BENKI ya Dunia imetoa Dola milioni 150 kati ya fedha ambazo imetenga kwa ajili ya miradi ya Msumbiji kusaidia kufadhili juhudi za taifa hilo la Kusini mwa Afrika kuokoa maisha ya watu kutokana na Kimbunga Freddy.
Kimbunga hicho kilikuwa na dhoruba mbaya zaidi Afrika katika miongo miwili iliyopita. Ilipitia Malawi, Msumbiji na Madagaska mwishoni mwa Februari kabla ya kuanza tena mwezi Machi. Zaidi ya watu 1,000 waliripotiwa kufariki katika maeneo hayo.
“Kipaumbele chetu ni kuunga mkono Serikali kujibu dharura hii haraka na kuhakikisha kuwa watu walioathiriwa na kimbunga wanaweza kupona haraka iwezekanavyo,” Xavier Chavana, mtaalamu wa usimamizi wa hatari za maafa nchini Msumbiji alisema katika taarifa yake.
Benki ya Dunia imesema fedha hizo zitaisaidia serikali ya Msumbiji kurejesha miundombinu ya usafiri na kutoa huduma zikiwemo za maji, usafi wa mazingira, afya na elimu.
Fedha hizo zinatokana na miradi iliyopo ya Benki ya Dunia nchini Msumbiji na ni tofauti na ruzuku ya $300m ambayo iliidhinisha mwezi Julai. Pesa hizo zinajumuisha $100m ya pesa ya ruzuku na $50m ya mkopo uliotolewa na benki.
Mwezi Machi, kimbunga hicho kilikumba eneo la kati la Msumbiji, na kuezua paa za majengo na kuleta mafuriko kuzunguka bandari ya Quelimane kabla ya kuelekea ndani kuelekea Malawi, ambako mvua kubwa ilisababisha maporomoko ya ardhi.