‘Wengi wamekutwa na magonjwa wasiyoyatambua’
IFAKARA, Morogoro: MKUU wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya amewaagiza watendaji wa vijiji, kata na maofisa maendeleo ya jamii wa tarafa na kata ndani ya Halmashauri ya Mji wa Ifakara, wilayani Kilombero kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kushiriki programu ya siku tano ya uhamasihaji, usajili na upimaji wa afya bure unaoratibiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kubaini hali zao za afya na kupata msaada zaidi.
Akizungumza leo Agosti 27 ndani ya Soko Kuu la Halmashauri ya Mji wa Ifakara alipotembelea kujionea utekelezaji wa programu hiyo inayojumuisha upimaji bure wa magonjwa ya shinikizo la damu, sukari, tezi dume pia uchunguzi wa Uwiano wa Urefu na Ufupi (BMI).
“Niombe Meneja wa Mkoa, NHIF Mbala Shitindi hawa maofisa maendeleo ya jamii upate muda nao kabla ya ijumaa (Agosti 30) kwanza waelewe somo kisha wakawe wahamasishaji kwenye kata zao ili wawe mabalozi wangu kwenye kata zao kama wataalamu wa maendeleo ya jamii,” ameagiza DC Kyobya.
SOMA: Watu 1,000 kufikiwa afya bure Ifakara
Katika hatua nyingine, Kyobya ameipongeza NHIF kuratibu programu hiyo ambayo imewasaidia wananchi zaidi ya 100 kupimwa na kutambua hali zao za afya.
“Wengi hatutambui hali zetu za afya, kweli au sio kweli? Hivyo ni muhimu kutambua hali zetu za afya ili kuchukua hatua za mapema,” amesema kiongozi huyo.
Kwa upande wake, Meneja wa NHIF Mkoa wa Morogoro, Mbala Shitindi amesema katika siku ya pili ya utekelezaji wa programu hiyo kwa kushirikiana na Kituo cha Afya cha Ifakara na Wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, wamewahudumia zaidi ya wananchi 250.
Akizungumzia juu ya zoezi la upimaji afya, Shitindi amesema kwa siku hizi mbili wamewapima wananchi 150.
“Wananchi 15 wamebainika na changamoto ya sukari. Wananchi 151 wamebainika kuwa na shinikizo la damu. Wananchi 10 wamebainika kuwa na changamoto ya tezi dume inayohitaji uchunguzi zaidi,” amesema.
SOMA: ‘Hakuna atakayekosa huduma NHIF’
Ameongeza, kati yao wamebaini wananchi wawili kuwa na changamoto ya mapafu yaani mfumo wa upumuaji na wananchi wanne wakiwa na changamoto ya moyo, hata hivyo wamewashauri wananchi hao kwenda hospitali kubwa wilayani humo kama Mtakatifu Francis na Hospitali ya Kansa ya Msamaria Mwema ‘Good Samaritan’ kwaajili ya uchunguzi na matibabu zaidi.
Amesema, huduma hii imewanufaisha wananchi kubaini changamoto zao pia ni sehemu ya maandalizi kuelekea utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote.