Wenye ulemavu waishukuru serikali utaratibu sensa

WALEMAVU wa viungo mkoani Mtwara, wameishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka utaratibu mzuri ambao umewawezesha kushiriki kikamilifu Sensa ya Watu na Makazi 2022.

Wakizungumza na Daily News Digital, baadhi ya walemavu wamesema walikuwa wanashindwa kushiriki kwenye mambo muhimu ya nchi ikiwemo sensa kutokana na imani potofu zilizosababisha wengi wao kufichwa.

“Utaratibu uliowekwa na serikali ya Rais Samia kuhusu walemavu kushiriki sensa  uko vizuri, hauna changamoto tunamshukuru sana,” amesema Said Hamisi.

Naye Hamis Ally, amesema kuwa amehamasika kushiriki sensa kutokana na utaratibu mzuri na hamasa ya Rais Samia kuwataka watu wote washiriku, wakiwemo wenye ulemavu, ili kuweka mipango mizuri ya maendeleo ya wananchi wake.

“Mimi nashukuru na nimefurahi kushiriki kwa sababu Mama ametuhamasisha, ni matarajio yetu kuwa atatupatia mikopo kwa ajili ya kuanzisha biashara maana wengine tunachoka kuombaomba,” amesema.

Mabruki Mohammed mmoja wa wananchi mkoani hapa amesema utaratibu  pamoja na hamasa ambayo imewekwa kwa sensa hii kushirikisha walemavu, uendelee kuwepo, ili na watu wenye ulemavu wasiwe wanabaki nyuma linapokuja swala la haki.

Mratibu wa Sensa Mkoa wa Mtwara, Tamali William amesema serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), walishirikisha kundi la walemavu kuanzia mwanzo wa uhamasishaji, ambao pia walishiriki katika mafunzo ngazi ya mkoa na wilaya.

“Tuna kundi la walemavu ambao walishiriki kikamilifu katika mafunzo ngazi ya mkoa na wilaya, ili wao wahamasishe wenzao kushiriki sensa na tunashukuru wengi wao wamefurahi na wanashiriki na kutoa taarifa zao bila kuficha,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button