Wenza wa Viongozi wawafariji waathirika maafa Hanang

MANYARA: Umoja wa Wenza wa viongozi “Ladies of New Millenium Women Group” wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyokabiliana mafuriko yaliyosabisha maporomoko ya tope kutoka Mlima Hanang, mkoani Manyara.

Akizungumza na waathirika katika kambi iliyopo shule ya sekondari Katesh, wilayani Hanang mkoani Manyara kwa mlezi wa umoja huo ambaye ni mke wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Mama Mary Majaliwa amesema kitendo cha Rais Dk. Samia kuacha majukumu yake tena akiwa nje ya nchi na kurejea kwenda kuwapa pole waathirika, ni kitendo cha upendo mkubwa alionao kwa Watanzania.

Mama Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na waathirika wa maafa hayo kwa niaba ya wenza wengine wa viongozi. Mafuriko hayo yamesababisha vifo vya watu 89 na wengine zaidi ya 600 kukosa makazi katika Wilaya ya Hanang mkoani Manyara.

Advertisement

“Tumeguswa sana na madhila yaliyowapata na tumekuja kuwapa pole lakini pia tumekuja kuungana na Rais, Dk Samia Suluhu Hassan na tunamshukuru kwa namna alivyoweza kukabiliana na matokeo ya janga hili na kuhakikisha waathirika wote wanapata huduma kwa haraka kwa kuleta Serikali yake hapa na tunashukuru kuona Hanang imetulia, na shughuli zinaendelea kuimarika.”

Msaada walioutoa ni pamoja na sare za shule 200, viatu jozi 216, madaftari 611, blanketi 105, mashuka 105, chupi za watoto 600, vitenge 40, kanga 100, mchele kilo 450 vifaa vingine na vyandarua, tisheti na taulo za kike.

“Muendelee kuishi kwa upendo, saidianeni kwa hali na mali huku mkimtanguliza Mungu kwa kila hali, pia tunaomba Serikali ikikamilisha miundombinu ya shule, iliyopata athari muwapeleke watoto shuleni, msiwaache nyumbani.”

Naye Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu Fredreck Sumaye mama Esther Sumaye ameishukuru Serikali kwa namna ilivyosaidia waathirika na kuomba waendelee na huduma kwa wathirika wachache waliobaki.

Awali akitoa taarifa ya janga hilo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga amesema idadi ya waathirika kwenye kambi imepungua kutokana na juhudi zilizofanywa na serikali kuwaunganisha waathirika na ndugu zao na kwenye kambi wamebaki waathirika 27.

“Tulikuwa tunakambi tatu za waathirika, moja ikiwa Ganana, Gendabi na Katesh na tulikuwa na waathirika jumla 683 na Serikali imekuwa ikiwahudumia tangu kutokea kwa janga hili, lakini kadri siku zinavyokwenda, baadhi ya waathirika walikuwa wakiomba kutoka baada ya kupata ndugu zao na waliosema wanataka kwenda Mwanza kwa ndugu zao, Serikali iliwagharamia”

 

2 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *