WHO yaombwa kusaidia mapambano dhidi ya Ebola

ILI kukabiliana na viashiria vya ugonjwa wa Ebola, Serikali ya Tanzania imeomba  msaada wa rasilimali fedha kwa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Pia serikali imeomba vifaa tiba, vifaa kinga pamoja wataalamu ikiwemo madaktari, wauguzi na watu wa maabara.

Akizungumza mkoani Kagera mara baada ya kukagua mpaka wa Kashenye na Nangoma, ambao una muingiliano mkubwa wa wananchi wa Uganda na Tanzania, Waziri  wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema tayari amewasilisha maombi hayo WHO, ambao wameahidi kuisaidia Tanzania katika mapambano hayo.

“WHO wamenihakikishia wapo stand by kutusaidia, wana wataalamu wazoefu ambao wamehudumu Liberia, Guinea na Uganda, wana wataalamu wa kutosha watusaidie, hii itawaondolea hofu hata madaktari wetu, wakikutana na daktari kashahudumia wagonjwa wa Ebola Guinea kwa miaka mitano, itamjengea ujasiri,” amesema.

Pia Waziri Ummy ameitaka WHO kuhimiza kampuni za chanjo, ili ziweze kutoa chanjo ya Ebola kama ilivyo ya Covid 19.

“Nimekutana na wataalamu wa WHO nchini, nimezungumza nao, nimewahimiza shirika na jumuiya za kimataifa  watusaidie katika mapambano hasa upatikanaji wa chanjo ya Ebola kwa haraka kàma ilivyo ya Covid 19.

“Shida iliyopo sasa, chanjo ya Ebola ya Zaire inayotolewa ni tofauti na ya Sudan,” amesema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila awali, akizungumza, amesema licha ya kutenga vituo 12 kwa ajili ya wagonjwa Ebola ikiwa ni mayarisho, ameiomba serikali kujenga majengo maalumu ‘Isolation’ matatu kwa ajili ya watu wenye magonjwa ya mlipuko katika eneo la Mrongo Wilaya ya Kyerwa na Ngara, ambako kuna mpaka wa Rusumo, Rwanda na Kabanga, Burundi.

 

Habari Zifananazo

Back to top button