Wizara ya Elimu kinara matumizi ya nishati safi ya kupikia

DODOMA: Taasisi za umma zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku kutoka katika wizara sita zimetekeleza maelekezo ya Serikali ya kuhama kutoka kwenye matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekuwa kinara kwa taasisi zake kutekeleza agizo hili la Serikali kwa zaidi ya asilimia 85.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk Selemani Jafo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa maelekezo ya usitishaji wa matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi za umma.

Amesema lengo la maelekezo hayo ni kupunguza madhara ya kiafya na mazingira yanayosababishwa na kukithiri kwa matumizi ya kuni na mkaa katika jamii zetu na ukataji wa miti kwa ajili ya nishati ya kupikia.

Amesisitiza kuwa katazo hilo haliwahusu watumiaji katika ngazi ya kaya na watumiaji wadogo bali limeanza kwa watumiaji wakubwa. Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waanze kutumia nishati safi ya kupikia.

“Kama nilivyosema hapo awali, katazo hili linazohusu Taasisi kubwa Taasisi hizo ziko chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Afya, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,” amesema Dk Jafo.

Dk Jafo amesema Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 inahimiza umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira ikiwemo rasilimali za misitu, hivyo ili kufikia lengo hilo, Sera inahamasisha matumizi ya nishati mbadala wa kuni na mkaa kwa lengo la kupunguza ukataji miti na uharibifu wa misitu.

Ameongeza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazoandaa na kulisha watu zaidi ya mia moja (100) kwa siku, ifikapo Januari 30, 2024 ambapo katika taarifa yake ya utekelezaji wizara hizo zimetuma mipango husika ya matumizi ya nishati mbadala na jinsi zitakavyotekeleza agizo hili.

Habari Zifananazo

Back to top button