Wizara yafuatilia dhahabu kilo 53 iliyodakwa India

Wizara yafuatilia dhahabu kilo 53 iliyodakwa India

RAIA wanne wa India wanaodaiwa kutoka Tanzania, wamekamatwa nchini humo wakiwa na kilo 53 za madini ya dhahabu.

Inadaiwa watuhumiwa hao walikamatwa Novemba 11, mwaka huu katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Chhatrapati Shivaji Maharaj (CSMIA) Mumbai.

Gazeti la Indian Express limewakariri maofisa wa kiwanja hicho wakidai kuwa watuhumiwa walikutwa na dhahabu ikiwa katika uzito wa kilo moja moja zilizofunikwa na mifuko kadhaa.

Advertisement

Inadaiwa watuhumiwa hao walizieleza mamlaka kuwa raia wa Sudan ambaye hawamfahamu, aliwapatia dhahabu hiyo wakiwa kwenye kubadili ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Doha, Qatar na hakusafiri nao.

Aidha, siku hiyo hiyo ya Novemba 11, maofisa wa CSMIA waliwakamata abiria watatu akiwamo mwanamke anayekaribia umri wa miaka 70, wakiwa na kilo nane za dhahabu na inadaiwa waliwasili hapo wakitoka Dubai.

Maofisa walidai kuwa dhahabu hiyo ilifichwa kwenye sehemu ya kiuno ya nguo za jeans walizokuwa wamevaa watuhumiwa na wamewekwa rumande kwa siku 14.

Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa alisema taarifa kuhusu kilo hizo 53 za madini ya dhahabu yanayodaiwa kutoka Tanzania wanazifuatilia.

Dk Kiruswa alisema hata Wizara ya Madini wamezisikia taarifa hizo lakini hawana hakika kama kweli ni madini kutoka Tanzania, hivyo wanafuatilia ili kujiridhisha ukweli wa taarifa hizo.

Mapema mwezi huu, maofisa wa forodha katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Indira Gandhi walikamata abiria watatu wakiwa na dhahabu yenye thamani ya dola za Marekani 369,000.

Hivi karibuni, maofisa katika Kiwanja cha Ndege cha Thiruvananthapuram Kusini mwa India walimkamata abiria akiwa na kilo moja ya dhahabu akitokea Dubai.

Mwezi uliopita, abiria aliyewasili katika Kiwanja cha Ndege cha Kochi akitoka Dubai, alikamatwa akitaka kutorosha dhahabu aliyoiweka kwenye taulo zilizowekwa kwenye dhahabu ikiwa kimiminika na aliiweka kama sehemu ya mizigo yake.