Wizara yapokea msaada mapambano ya Ukimwi
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imepokea vitendea kazi vyenye thamani ya Sh milioni 800 kutoka kwa wadau wa CDC kupitia THPS kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI na kifua kikuu katika Mkoa wa Tanga.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amepokea vitendea kazi hivyo leo Februari 23, 2024 mkoani Tanga ambavyo ni pikipiki 50, friji 72, centrifuges 56, compyuta 50, UPS 50 na printa 50 ambavyo vitaimarisha huduma za afya mkoani humo.
Wakati akipokea vitendea kazi hivyo, Waziri Ummy amewataka wote watakaokabidhiwa vifaa hivyo kuvitumia kama ilivyoelekezwa ikiwa ni pamoja na kuwafikia wateja wanaoishi katika mazingira magumu na mbali na vituo vya kutolea huduma za afya ili kuwafikishia huduma.
“Lakini pia tunaamini kwamba mtaongeza idadi ya huduma mkoba ‘outreach services’, kuwafikia wateja walio katika mazingira hatarishi ya kuambukizwa ugonjwa wa UKIMWI na kuwapatia huduma za kinga zikiwemo kinga dawa na kusafirisha sampuli kwa ajili ya kupima wingi wa Virusi vya UKIMWI.” Amesema Waziri Ummy.
Pia, amewataka kutunza vifaa hivyo na kuvifanyia matengenezo ya mara kwa mara ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kutimiza lengo la kudhibiti UKIMWI na VVU ambapo ametoa onyo kwa yeyote atakae fanya kinyume na maelekezo hayo kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Mkurungenzi Mtendaji wa THPS Dk Redempta Mbatia amesema kuwa msaada ni sehemu ya juhudi ya kuongeza ufanisi na ubora wa huduma jumuishi za Kinga ,matunzo na matibabu ya VVU mkoani Tanga.
“Tunaamini vifaa tulivyokabidhi leo vitatumika Kwa malengo yaliyokusudiwa hivyo kuchangia kuongeza ufanisi na ubora wa huduma za afya Kwa jamii”amesema Dk Mbatia