WLF yajizatiti kumaliza tofauti za kiitikadi kwa wanawake

GEITA: JUKWAA la Viongozi Wanawake (WLF) limetangaza kuja na mipango mikakati inayoazimia kuunganisha makundi yote ya wanawake pasipo kujali tofauti za kiitikadi za dini, siasa na elimu.
Mwakilishi wa WLF, Evelyne Munisi amebainisha hayo katika hafla ya kilele cha siku ya wanawake duniani mkoa wa Geita iliyoambatana na uzinduzi wa mradi wa PAMOJA kitaifa.
Amesema WLF inaundwa na wanawake kutoka vyama tofauti vya kisisasa vyenye itikadi tofauti kwa kuwa dhamira yake ni kuinua na wanawake wa makundi yote bila kujali itikadi zao.

Evelyne ametaja ajenda na maazimio ya WLF ni kulinda heshima na hadhi ya mwanamke, azimio la sifuri dhidi ya ukatili, haki na afya kwa wanawake na haki na usawa maeneo ya kazi na uongozi.
Amesema WLF imejizatiti pia kusimamia uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kupitia taasisi za kifedha sambamba na kuunda umoja wa kitaifa, amani na mshikamano kupitia wanawake.
Amesema WLF imejipanga kuhakikisha wanawake wanaendelea kupata fursa kwenye sekta zote za kiuchumi bila kujali jinsia yao na kumfanya mwanamke kuwa mhimili wa maendeleo nchini.
Evelyne amesema WLF inalenga kuweka usawa katika nyanja zote katika mifumo ya maamuzi na uchumi wa kaya ikiwa ni safari ya dhati kuelekea 50 kwa 50 kati ya mwanaume na mwanamke.

“Rai yangu kwa wanawake, tuungane tuwe sauti moja kwa ustawi wetu na taifa letu lakini niwakumbushe kuwa WLF itabaki kuunganisha na siyo kugawa watu.
“WLF ni jukwaa la kusimamia maslahi ya taifa kwa kuunga mkono juhudi zinazogusa maisha ya mwanamke ikiwemo M-MAMA, fursa za elimu na ujuzi ili hatua ziendelee kuimarishwa zaidi” amesema Evelyne.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Zawadi Amour Nassour ameomba mbali na uwezeshaji unaofanyika wanawake waendelee kuheshimu nafasi ya mwanaume katika familia.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima ameahidi serikali itaendelea kushirikisha wadau wote ili kufanikisha matokeo chanya ya uwezeshaji wanawake.



