…Yafunguka maeneo ya reli za juu Dar, Dodoma

SERIKALI imesema inakamilisha maandalizi ya kuanza ujenzi wa treni za mjini zitakazopita juu katika majiji ya Dodoma na Dar es Salaam. Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema hayo wakati alipozungumza na waandishi wa habari jijini  Dar es Salaam .

Msigwa amesema kwa Dar es Salaam treni hizo zitaanzia Kawe, Mwenge, Mlimani City, Ubungo kisha kuelekea Kariakoo na kuunganishwa na reli ya kisasa (SGR). Amesema kutakuwa na tawi jingine kutoka Barabara ya Bibi Titi kwenda Morocco kupitia Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kisha kuunganisha Mwenge.

Msigwa amesema hiyo itakuwa awamu ya kwanza na kila baada ya kilometa mbili kitawekwa kituo ili Mkoa wa Dar es Salaam pekee uwe na mtandao wa kilometa 160. “Tutakuwa na treni kama hizi katika Jiji la Dodoma zitakazoanzia Stesheni ya reli ya kisasa (SGR) kwenda mjini, kisha tutaunganisha kwenda Mtumba hadi Chamwino na kwenda stendi ya mabasi.

Awamu ya pili itaelekea kiwanja cha ndege cha Msalato lengo letu katika mkoa huu ni kujenga kilometa 105 za mtandao wa treni za mjini, je mnafikiri watapenda hayo,” alisema. SOMA: SGR Uvinza-Musongati, funguo muhimu milango mipya ya uchumi

Msigwa amesema mradi wa vipande vinane vya mradi wa SGR unaendelea vizuri ikiwemo ya kuanzia Makutupola–Isaka na kwingineko. “Kazi inaendelea vizuri katika vipande vyote vinane kuanzia Makutupola-Tabora, Tabora-Isaka, Isaka-Mwanza, Tabora-Kigoma na kwenda Burundi. Tayari tumeanza kuvuka mipaka na sasa hivi tupo kwenye maandalizi ya ujenzi wa reli mpya,” alisema.

Ameongeza : “Tutajenga njia ya Kaskazini kwa maana ya Tanga, Arusha na Musoma kwa kilometa 1,028. Kusini eneo la Mtwara-Mbamba Bay kilometa 1,000 ili tuunganishe mzigo kutoka Bahari ya Hindi uvuke Ziwa Nyasa uende Malawi na nchi zingine, waseme wasiseme tutajenga”.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button