Yanga 1 USM Alger 2
NI matokeo ambayo hayakutarajiwa na wengi, lakini ndivyo ilivyo dakika 90 zimemalizika kwa USM Alger kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam,mchezo wa fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ikicheza mbele ya maelfu ya mashabiki waliojitokeza uwanjani, Yanga ilienda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0 lililofungwa na Aymen Mahious dakika ya 32, kabla ya Fiston Mayele kusawazisha dakika ya 82.
Hata hivyo furaha za mashabiki wa Yanga hazikudumu kwani dakika ya 84 Islam Merili, alifunga bao la pili na kuwapa wakati mgumu Watanzania waliokuwa uwanjani na waliokuwa wakifuatilia mchezo huo kwenye televisheni au mitandao ya kijamii.
Kwa matokeo hayo Yanga italazimika kushinda angalau mabao 2-0 zitakaporudiana wiki ijayo nchini Algeria ili iweze kutwaa kombe hilo.