Yanga yaandika historia nyingine

DAR ES SALAAM – YANGA jana imeandika historia nyingine kwa kuzindua Kitabu cha Historia ya Klabu hiyo tangu ilipoanzishwa Februari 11 mwaka 1935.

Kwenye hafla hiyo iliyofanyika Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali na wachezaji wa zamani wa klabu hiyo Rais wa Klabu hiyo Hersi Said alisema wameona huu ni wakati sahihi wa kuandika historia ya klabu hiyo kitakachokuwa na taarifa zote tangu ilipoanzishwa.

Hersi alisema Yanga imepitia vipindi mbalimbali vyenye furaha na kusikitisha hivyo wameona ni wakati sahihi kuandika kitabu cha historia ya klabu hiyo kwa ajili ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Advertisement

“Ndani ya kitabu hiki yapo mambo mazuri, lakini pia yapo mambo ya kuhuzunsha kwenye historia ya klabu hii iliyoanzishwa mwaka 1935.

Tumeona muda unapita na watu wengine wenye historia ya klabu hii wameanza kufariki, hivyo tumeona huu ni wakati sahihi wa kuwapata watu wenye historia ya klabu hii walio hai kupata taarifa zake,” alisema Hersi.

Alisema wamepata taarifa za historia ya Yanga kutoka makataba mbalimbali lakini pia kutoka kwa watu mbalimbali waliopita kwenye klabu hii kuanzia viongozi, wachezaji na hata wahariri wa habari waliokuwepo nyakati hizo.

“Katika kufanikisha kupata taarifa hizo muhimu tulilazimika kusafiri kwenye sehemu mbalimbali, tulienda Zanzibar, Mwanza, Morogoro, Mtwara na sehemu nyingine ambazo walitupa historia ya klabu hii na kuziunganisha kupata kitabu hiki tunachokizundua leo,” alisema Hersi.

Hersi alisema walitumia kipindi cha miezi 10 kuandika kitabu hicho ambacho alisema watakisambaza kwa namna tofauti tofauti na kukiuza. Akizungumza kwenye tukio hilo Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Leodeger Tenga ambaye alialikwa kama mchezaji wa zamani wa Yanga alisema klabu hiyo imefanya jambo jema linalopaswa kuigwa na klabu nyingine.

SOMA: Mapya: Simba waanza kufungiana

“Sikuwa nimejua kama nimealikwa kama mchezaji wa klabu hii, waliniambia kuwa tumekualika kama mchezaji, nikasema kumbe na mimi nimewahi kucheza Yanga. Niseme ni jambo zuri linaposwa kuigwa na klabu nyingine,” alisema Tenga.

Nyota wengine wa zamani wa Yanga waliokuwepo kwenye uzinduzi hiyo kuwataja kwa uchache ni Sekilojo Chambua, Omary Hussein, Makumbi Juma, Seleman Jongo, Shaabani Katwila, Ahmedi Amasha, Abeid Mziba, Juma Pondamali ambao wote walimsifu Hersi kwa kuandaa kitabu hicho.