Yanga yarudisha pesa, Feisal aaga rasmi yani utata mtupu
KLABU ya Yanga imethibitisha kupokea barua kutoka kwa mchezaji Feisal Salum Abdallah Disemba 23, 2022 inayoeleza kuvunja mkataba wake baina yake na klabu.
Baada ya kupokea barua hiyo Yanga imesema hakuna misingi ya kikanuni wala kisheria kulingana na mkataba wake ambazo zinampa haki mchezaji kusitisha mkataba wake na Klabu kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba wa sasa. “Kanuni na Taratibu za FIFA ziko wazi na zimeelezea taratibu zote juu ya Jambo la aina hii.” imeeleza taarifa ya Yanga.
Yanga imesema kuwa mkataba baina ya mchezaji na Klabu hauwezi kuvunjwa na upande mmoja tu bila kujadiliana na upande wa pili wakati msimu wa ligi ukiwa unaendelea. Imeeleza kuwa kwa mazingira hayo, barua ya mchezaji ina dhana potofu na haina misingi ya kisheria ya kuvunja mkataba baina ya klabu na mchezaji.
Yanga imeeleza kuwa imemuagiza Feisal, azingatie matakwa ya mkataba wake kama ilivyoelezwa katika mkataba huo. Klabu pia imemkumbusha Feisal, mkataba wake wa sasa ni halali hadi ifikapo Tarehe 30 Mei 2024.
Yanga imesema inathamini kiwango na mchango wa Faisal na tayari walishaanza mazunguzo na wawakilishi wa Feisal wakiongozwa na mama mzazi wa mchezaji ili kuboresha maslahi yake na kuongeza muda wa mkataba wake wa sasa ambao unaishia Mei 2024.
“Hata hivo, Klabu haijapokea majibu mbadala wa mapendekezo ya maboresho haya kutoka upande wa Feisal na wawakilishi wake na badala yake tumepokea barua inayoelezea kuvunja mkataba kutoka upande wa Feisal ambayo ni Kinyume na makubaliano ya mkataba wake wa sasa.” imeeleza taarifa hiyo.
Klabu tayari imesharejesha fedha kiasi cha TZS 112,000,000 (Millioni Mia Moja na Kumi na mbili) ambazo Feisal aliziweka katika Akaunti za Klabu.
“Tunapenda kueleza kuwa, kuna taratibu na kanuni za Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) na zile za Shirikisho la Mpira wa miguu Duniani (FIFA) ambazo ni lazima zifuatwe na timu yoyote ile inayotaka kumsajli mchezaji yeyote wa Klabu ya Young Africans SC (YANGA).” inaeleza taarifa.
Yanga, inasisitiza kuwa, Feisal Salum Abdallah ni mchezaji halali ya Yanga na ana mkataba hadi kufikia Mei 30, 2024.
Hata hivyo baada ya tetesi hizo kiungo huyo ameiaga timu hiyo na mashabiki kwa ujumla katika kipindi chote alichoitumikia timu hiyo yenye maskani yake Jangwani.
Mpaka sasa sio Azam FC, wala Yanga waliothibtisha kuuziana mchezaji huyo mzaliwa wa Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa na kiungo huyo imeeleza kuwa baada ya kukaa pamoja kwa kipindi kirefu sasa ni wakati wa kuwaaga, ingawa haikueleza ni wapi anaelekea.
“Nitakumbuka mengi mazuri tukiwa pamoja na nitasahau mabaya yote kwa haraka sana.” ameandika Feisal kupitia taarifa yake.