Zahanati yafungwa kwa kukosa watumishi

MADIWANI  wa Halmashauri ya  Wilaya ya Shinyanga  wamelalamikia hatua ya zahanati ya  Kijiji cha Bugogwa iliyopo kata ya Mwamala  kufungwa kwa muda wa mwaka mmoja,  kutokana na kukosa watumishi wa afya.

Diwani Viti Maalum, Anna Pius ametoa ripoti hiyo  leo kwenye kikao cha kawaida cha baraza la madiwani cha robo ya tatu ya mwaka na kujadiliwa na madiwani wote na kutaka Mkurugenzi Nice Munisy aeleze kuhusu jambo hilo.

Pius ameeleza  kufungwa huko kulitokana na daktari aliyekuwepo kwenye zahanati hiyo kufariki  na kubaki muuguzi peke yake ambaye alidai hawezi kuwapa huduma wala kujaza madokezo.

“Wananchi sasa hivi wanapata huduma kwenye zahanati ya Kijiji cha Mwamala na kituo cha Afya Samuye,”amesema Pius.

Diwani  wa Kata ya Itwangi Sonya Mhela, amesema taarifa hiyo waliipata kutoka kwa wananchi  wa eneo hilo na kuanza kufuatilia  na kugundua kituo kimefungwa.

Diwani wa Kata ya Salawe na diwani wa Kata ya Ilola Amos Mshandete,  wamesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitafuta fedha ili kuwaondolea changamoto wananchi  kupata huduma za afya, lakini ni aibu zahanati kufungwa  na watoto wamekuwa wakisumbuka kupata chanjo.

“Tunaomba mganga mkuu wa halmashauri atuombe radhi baraza kwani taarifa hii Mkurugenzi amedai haifahamu,  ikiwa kila siku inatakiwa kuripoti taarifa kwa mkurugenzi afahamu na achukue taarifa,”alisema Mshandete.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Nice Munisy alisema taarifa ya kufungwa kwa zahanati hiyo hana.

Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo,   Nuru Yahya alikiri kufungwa kwa zahanati hiyo, huku akieleza daktari aliyekuwepo alifariki na muuguzi kupata changamoto ya kifamilia,  hivyo siku ya Jumatatu itapata mtumishi ambaye atatoka kituo cha Afya Samuye,  huku akiomba radhi kwenye baraza hilo.

Habari Zifananazo

Back to top button