Zaidi ya leseni 1,000 za madini zatolewa Kahama

KAHAMA: HALMASHAURI tatu za Mkoa wa Kimadini Kahama, Ushetu, Msalala na Kahama zimetoa jumla ya leseni 1356, huku fursa za uwekezaji zikiendelea kukuzwa.
Afisa Madini Mkazi wa Kahama, Leons Welengeile, amesema leseni 77 za utafutaji madini, hasa dhahabu, zimetolewa, na shughuli kubwa zinafanyika katika migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi, ingawa mgodi wa Buzwagi upo hatua za ufungaji.
Katika mgodi wa Buzwagi, maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na taasisi za elimu yamewekwa, huku takribani kilomita 13 za mraba zikitengwa kwa shughuli mbalimbali za viwanda.
Pia, leseni saba za uchimbaji wa kati zipo, na leseni nne ziko kwenye hatua ya uendelezaji. SOMA: Kahama kinara utoroshaji madini
Kwa hadi Februari 2025, leseni 1270 za uchimbaji mdogo zimetolewa, ambapo asilimia 40 zimeendelezwa na asilimia 60 zipo kwenye hatua za utafiti.
Mkoa huo pia unatoa fursa katika biashara ya madini, ujenzi wa mitambo ya uchenjuaji madini, na miradi ya msaada wa kiufundi kwa wachimbaji wadogo.
Kwa sasa, uzalishaji wa dhahabu umeongezeka kwa maeneo ya Shangaza, LHT, na Super Mabomu, baada ya uwekezaji wa mikataba ya msaada wa kiufundi.